JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. PROF.
IBRAHIM HAMIS JUMA AKIWA PAMOJA NA WAKANDARASI WA KAMPUNI YA MASASI
CONTRUCTION LTD. WANAOJENGA JENGO LA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA
KIGOMA. MAHAKAMA YA TANZANIA INAJENGA JENGO HILI PAMOJA NA MENGINE
NCHINI ILI KUSOGEZA HUDUMA ZA MAHAKAMA KARIBU ZAIDI NA WANANCHI.
JENGO LA MAHAKAMA KUU KANDA YA KIGOMA LIKIWA LIMEFIKIA HATUA HIYO
………………
Na Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kuishirikisha Mahakama ya
Tanzania kwenye mipango yake ya uanzishaji wa maeneo mapya ya kiutawala
ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake
mjini Kigoma, Jaji Mkuu amesema mipango ya Serikali ya uanzishwaji wa
wilaya au mikoa izingatie pia uanzishwaji wa Mahakama. Aliongeza kuwa
Mikoa na wilaya mpya ndizo zenye ukosefu wa Mahakama hali inayowafanya
wananchi kufuata mbali huduma za kimahakama.
Alisema Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16 hadi 2019/20)
imejipanga kutatua tatizo la ukosefu wa huduma za Mahakama pamoja na
kusogeza huduma hizo karibu Zaidi na wananchi. Kwa kushirikiana na Benki
ya Dunia, tayari imeanza ujenzi wa Mahakama tano za Hakimu Mkazi katika
mikoa ya Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Manyara pamoja na ujenzi wa
Mahakama 16 za wilaya na Mahakama Kuu mbili katika Mikoa ya Kigoma na
Mara.
Jaji Prof. Juma amesema kupitia
ziara yake ya siku saba kwenye Mahakama Kuu kanda ya Tabora amebaini
kuwa watanzania wengi hufuata mbali huduma za Mahakama na maeneo mengine
ni kutokana na jiografia ya maeneo hayo. Akitolea mfano wa wilaya ya
Uyui mkoani Tabora, Jaji Mkuu amesema kutokana na wilaya hiyo kuzunguka
mkoa, wananchi wake hulazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu zilizopo
umbali wa Zaidi ya kilometa 377.
Alisema Mahakama itaanzisha
Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) kwenye maeneo yote yenye
changamoto kama hizo kabla ya kujenga Mahakama kwa kuwa changamoto ya
upatikanaji wa huduma za kimahakama bado ni kubwa nchini.
Kuhusu utendaji kazi, Jaji Mkuu
aliwapongeza watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora kwa kubuni
mkakati wa kupunguza mlundikano wa kesi kwenye Mahakama zake. Kanda ya
Tabora ndiyo kanda pekee nchini iliyopunguza siku za mpango wa upimaji
wa kumaliza mashauri Mahakamani kutoka miaka miwili mpaka moja kwa kesi
za Mahakama Kuu, miezi sita badala ya 12 kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na
wilaya na kutoka miezi 6 mpaka 3 kwa kwa Mahakama za Mwanzo.
Katika kipindi cha mwezi Januari
hadi Disemba 2017, kanda ya Tabora ilisajili jumla ya mashauri 1112 na
mashauri yaliyosikilizwa na kumalizika yalikuwa 1194 wakati mashauri
yaliyobaki Desemba 2016 yalikuwa ni 541.
Aidha Kanda ya Tabora imemaliza
mashauri ya mlundikano kwa kiasi kikubwa hivyuo kufanya mashauri hayo
kwisha kabisa katika Mahakama za Mwanzo na kupungua kwa kiasi kikubwa
katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya. Mashauri ya
mlundikano yaliyobaki Mahakama Kuu hadi kufikia Desemba 31 yalikuwa 4.
Kati ya mashauri hayo, mashauri
yenye umri kati ya miezi 25-48 Mahakamani yalibaki 3 na shauri moja (1)
lenye umri wa miaka 5-10 lilibakia. Aidha, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora
haina mashauri yenye umri wa Zaidi ya miaka 10.
Jaji Mkuu amemaliza ziara yake ya
siku saba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora ambapo
alikagua shughuli mbalimbali za Mahakama pamoja na kuwatembelea baadhi
ya wadau wa Mahakama wakiwemo wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujadiliana
na viongozi hao namna ya kupunguza changamoto zinazoikabili Mahakama ya
Tanzania pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau hao.
No comments :
Post a Comment