Mkurugenzi wa kampuni ya Global
Land Solution ,Zainuddin Adamjee, (mwenye kibagharashia )akimtembeza
mkuu wa mkoa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, katika fukwe ya bahari
kwenye eneo la uwekezaji wa masuala ya utalii Palacha (dream
city)kijiji cha Mpafu-Mkuranga,ambako kunatarajia kuwa mji wa kisasa
ukitoa huduma za kitalii kupitia fukwe za bahari .(picha na Mwamvua
Mwinyi)
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi
Evarist Ndikilo (kushoto) akionyeshwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni
ya Lodhia Group of Companies ,Mkuranga ,anaemuonyesha bidhaa hizo
ni mkurugenzi wa kampuni hiyo ,Arun Lodhia.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi
Evarist Ndikilo (kushoto) akitembelea kampuni ya Lodhia Group of
Companies ,Mkuranga inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali
za chuma na plastiki, wa (kulia) ni mkurugenzi wa kampuni hiyo Arun
Lodhia.(picha na Mwamvua Mwinyi)
……………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
MKOA wa Pwani, unatarajia
kuzindua viwanda Tisa ambavyo vimeshakamilika, ikiwa ni muendelezo wa
kasi ya kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji katika mkoa huo.
Aidha imewaelekeza wakuu wa
wilaya na wakurugenzi wa mkoa huo, kuhamasisha wawekezaji
watakaoweza
kwenda kuwekeza kwenye eneo la sekta ya utalii hasa kwenye fukwe
zilizopo mkoani humo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi
Evarist Ndikilo, aliyasema hayo wakati alipotembelea baadhi ya viwanda
pamoja na eneo la uwekezaji wa masuala ya utalii eneo la Palacha,kijiji
cha Mpafu-Mkuranga.
Alisema wanatarajia kuzindua
viwanda hivyo,wakati wowote kuanzia sasa ,ikiwa ni sanjali na kiwanda
cha Sayona-Lugoba, Twyford kilichopo Pingo,KEDS na viwanda vitatu
vinavyondeshwa na kampuni ya Lodhia Group of Companies inayojihusisha na
utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za chuma na plastiki iliyopo
Mkuranga.
Mhandisi Ndikilo, alieleza
wamejipanga kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda hivyo kukamilika kwa
viwanda hivyo inawapa imani ya kutimiza adhma ya mkoa huo kuwa ukanda wa
viwanda.
Alielezea wanatekeleza sera ya
ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,kwa vitendo ambapo kwasasa kuna
viwanda zaidi ya 300 ambavyo viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji
na vingine vimeshaanza uzalishaji.
“Tunashukuru kuona wawekezaji
wameboresha yale yote waliyotakiwa kuyafuata na kukamilisha ujenzi kwa
asilimia 90, kwani viwanda vyote vikianza uzalishaji vitasaidia
kuliingizia pato Taifa na kuwa mkombozi katika eneo la ajira.”alisema
mhandisi Ndikilo.
Pamoja na hayo, mkuu huyo wa mkoa , aliziasa taasisi wezeshi
ikiwemo Dawasco, Tanesco, TARURA na halmashauri mbalimbali kushirikiana
na wawekezaji kwenye maeneo yao na kuondoa urasimu .
“Matarajio yetu ni kupanua wigo katika ajira ,kuondokana na
umaskini kwani wananchi watapata kazi na wengine wataanzisha huduma
ndogondogo kwa wafanyakazi kwenye viwanda hivyo,” alisema mhandisi
Ndikilo.
Hata hivyo, mhandisi Ndikilo
alisema uendelezaji wa maeneo ya utalii utavutia watalii wengi na
kuingiza mabilioni ya fedha kutokana na kodi na wageni kutoka nje.
Akielezea eneo la Palacha,
alieleza itasaidia kuanzishwa kwa huduma za kijamii kama vile uwanja wa
ndege, mahoteli, masoko na shule ambapo watalii watakuwa wakifanya
shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuogelea, uzamiaji na michezo
mingine ya baharini.
Nae mkurugenzi wa kampuni ya
Global Land Solution ,Zainuddin Adamjee,aliushauri mkoa wa Pwani,
kuunda kamati ndogo ya mamlaka ya kuratibu uwekezaji kwenye fukwe ili
kurahisha kukuza Utalii wa fukwe nchini.
Alisema kuwa ,wameanzisha mradi wa Palacha Dream City ambao ni
mji utakaokuwa wa kisasa ukitoa huduma za kitalii kupitia fukwe za
bahari zenye urefu wa kilometa nne,huko kijiji cha Mpafu ,Mkuranga.
“Mradi huu ulibuniwa miaka minane
iliyopita ili kuchangia katika uendelezaji wa sehemu za utalii katika
ukanda wa kusini na kuinua uchumi wa mkoa huo.”
“Mradi utakapokamilika utakuwa
kiuongo muhimu cha sehemu zote za utalii katika ukanda wa kusini kwani
utakuwa na kiwanja cha ndege ambacho mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania
imeshakipitisha”alisema Adamjee.
Adamjee alielezea ,mradi huo
unahitaji umeme mwingi hivyo wanaiomba REA awamu ya tatu iwafikie na
huduma ya maji ya uhakika katika kijiji cha Mpafu eneo la Palacha na
maji ya uhakika.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa
kampuni ya Lodhia Group of Companies ,inayojihusisha na utengenezaji wa
bidhaa mbalimbali za chuma na plastiki ,Arun Lodhia, alieleza wameshatoa
ajira ya watu 1,500 wakiwemo vijana.
Alisema, mbali ya ajira hizo pia wameweza kujenga barabara ambayo inatumiwa na wananchi wanaozunguka kiwanda hicho.
“Tunaomba tupatiwe umeme wa
uhakika na kuunganishwa kwenye gridi ya taifa ili kuwa na umeme wa
uhakika ambao utasaidia kwenye shughuli zetu,” alisema Lodhia.
No comments :
Post a Comment