Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu)
Mhe.Jenista Mhagama akitoa tamko la Serikali leo mjini Dodoma kuhusu Kusitishwa
kwa Shughuli za Kampuni zinazotoa huduma ya Uwakala Binafsi wa Ajira baada ya
kukiuka sheria ni pamoja na Sasy Solution
Company Ltd, Bravo Job Centre Agency na Competitive
Manpower International Ltd ambapo Kampuni hizo haziruhusiwi kujihusisha na
shughuli za Uwakala Binafsi wa
Ajira nchini, Januari 25, 2018.
NA MWANDISHI WETU.
SERIKALI yasitisha Shughuli za Kampuni Tatu (3) za Wakala Binafsi wa
Huduma za Ajira hapa Nchini kutokana na kukiuka matakwa ya sheria ya Huduma za
Ajira Na.9 ya mwaka 1999 na Kanuni zake.
Akitoa tamko la Serikali kuhusu Kusitishwa kwa Shughuli za Kampuni hizo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama amesema
kuwa Ofisi yake imekuwa ikipokea ...malalamiko kutoka kwa wafanyakazi na wadau
mbalimbali kuhusu utaratibu unaotumiwa na baadhi ya Wakala Binafsi wa huduma za
Ajira nchini.
Kampuni zilizofutiwa usajili baada ya kukiuka sheria ni pamoja na Sasy
Solution Company Ltd, Bravo Job Centre Agency na Competitive Manpower
International Ltd ambapo Kampuni hizo haziruhusiwi kujihusisha na shughuli
za Uwakala Binafsi wa Ajira nchini.
Akifafanua Mhe. Mhagama amesema kuwa uchunguzi umebaini ukiukwaji wa
taratibu za usajili ambapo baadhi ya Mawakala wamekuwa wakitumia nyaraka
zilizopatikana kwa njia isivyo halali katika kujipatia leseni za uwakala hali
iliyowawezesha kukwepa kodi na kujipatia faida.
Aliongeza kuwa ukiukwaji wa taratibu za kisheria umeleta athari mbalimbali
kwa wafanyakazi hasa kwa wale wanaoenda kufanya kazi Mataifa ya Nje ambapo
wafanyakazi hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji katika
ajira, malipo ya mishahara na stahiki mbalimbali.
Aidha, Mhe. Mhagama amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imesitisha mara moja
shughuli za Mawakala Binafsi wa huduma za Ajira zinazohusika na kuwatafutia
kazi wafanyakazi nje ya nchi (cross border placement) hadi hapo Serikali
itakapoleta mfumo wa kusimamia jambo hili na kutoa taarifa kwa umma.
Vile Vile, Waziri Mhagama amemwagiza Kamishna wa Kazi kuhakikisha kuwa
ndani ya wiki mbili kuzifanyia uhakiki Wakala zote zilizosajiliwa kuona kama
wametimiza na kuzingatia Sheria na Kanuni zinazosimamia Wakala Binafsi za
Ajira, Pia aliiasa Timu ya wakaguzi itakayoundwa na Wizara ikikiuka miiko ya
ukaguzi na kuficha udhaifu wa mawakala hao hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa
Mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.
No comments :
Post a Comment