Wednesday, January 31, 2018

MAWAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO WA TANZANIA NA RWANDA WAJADILI UJENZI WA RELI YA ISAKA- KIGALI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania Bw. Doto James (kulia) na mwenzake wa Rwanda Bw. Caleb Rwaunganza wakibadilishana taarifa walizosaini za maagizo kutoka kwa Mawaziri wa Wizara hizo mbili kuhusu hatua zaupatikanaji wa Fedha za mradi wa Reli ya Isaka Shinyanga hadi Kigali nchini Rwanda Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, WFM
Mawaziri wa Fedha na Mipango wa  Tanzania na Rwanda wamekutana  Jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kupata fedha za Ujenzi wa Reli yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda ikiwa ni mwendelezo wa mikutano kuhusu suala hilo iliyoanza kuanzia Januari 20, 2018.
Katika Mkutano huo wamejadili kuhusu njia ambayo inaweza kuwa rahisi kupata fedha ikiwemo ya kutumia Sekta binafsi, Serikali kukopa au kumweka mwekezaji ambapo wamekubaliana kupitia upya taarifa zilizo wasilishwa mezani za pande hizo mbili  na kufanya maboresho na pia kuzungumza na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa pamoja ili wakati wa kikao kijacho waweze kujadili suala hilo kwa kuangalia vigezo na masharti ya kupata fedha.
Kikao hicho ambacho ni cha watalamu kimewakutanisha Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri kutoka Rwanda Mhe. Gatete Claver pamoja na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura na Makatibu wakuu wa wizara hizo na wajumbe wengine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania Bw. Doto James na mwenzake wa Rwanda Bw. Caleb Rwaungaza, wamesaini maagizo hayo ya Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.
Ikumbukwe kuwa mapema mwezi huu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Rwanda Paul Kagame walikubaliana kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa Reli kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda na wakatoa maagizo ya kuanza utekelezaji kwa kuangalia namna ya kupata fedha za mradi huo.

No comments :

Post a Comment