Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa wajumbe wa
Bodi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo Mhandisi Deusdedit Kakoko, kukamilisha Skana mpya (haipo pichani),
ambayo inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Bandarini
hapo ambayo haijakamilika hadi sasa.
Muonekano wa Skana mpya ambayo
inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA), ambayo haijakamilika hadi sasa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Profesa
Ignatus Rubaratuka (Wakwanza kushoto), wakati akikagua shehena ya kahawa
iliyohifadhiwa Bandarini hapo kwa muda mrefu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikagua shehena ya kahawa
iliyohifadhiwa tangu mwaka 2014 hadi sasa katika ghala iliyopo katika
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dar es Salaam. Pembeni yake ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Profesa Ignatus
Rubaratuka akishuhudia ukaguzi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari Tanzania(TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, akifafanua jambo kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
alipofika Bandarini hapo leo wakati wa ziara ya kushtukiza kuangalia
uendeshaji wa huduma Bandarini hapo.
……………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema anasikitishwa na utendaji wa
Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kutofanya
maamuzi kwa wakati hali ambayo inachangia malalamiko kuongezeka
Bandarini hapo.
Aidha, Mbarawa amesema
Serikali inapeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya wa shughuli za Uendeshaji
Bandarini hapo kutokana na aliyekuwepo kushindwa kusimamia majukumu yake
ipasavyo.
Profesa Mbarawa amesema hayo leo
wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya bandarini ikiwa ni siku chache
baada ya Rais John Magufuli, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya
ziara ya kustukiza na kubaini madudu bandarini hapo.
Ziara ya Waziri Mbarawa ni
mwendelezo wa ziara mbalimbali bandarini hapo kubaini uendeshaji na
utendaji wa shughuli zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
“Nimelazimika leo kuwaita
Watendaji na Bodi ya TPA ili kuwaeleza kasoro zenu ambapo inaonesha
wazi kuwa asilimia kubwa ya mambo yanayotokea humu ni kuwa mnakuwa
wazito katika kutoa maamuzi”, amesema Profesa Mbarawa.
Amesema katika bandari hiyo ipo
mizigo ya kahawa ambayo imefika bandarini tangu mwaka 2014 huku kukiwa
hakuna sababu za kueleweka za wenye mali kutochukuwa mizigo yao.
Profesa Mbarawa amesema hahitaji
wasaidizi ambao wanakaa katika vikao na kulipana posho ila wanapaswa
kufanya kazi ya kuangalia shughuli zote za bandari.
“Kama hamtabadilika nitaendelea
kuja katika bandari hii ili kuchukua hatua pale ambapo inaonekana kwani
haipendezi kila kukicha malalamiko kutokea,” amesisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa ameitka bodi
na menejimenti kuhakikisha kuwa inatatua changamoto iliyopo katika
bandari ya kushusha na kupakia mizigo kutoka Zanzibar na kuingia
Tanzania Bara ambapo wafanyabiashara wanalalamikia utaratibu unaotumika
kuwahudumia.
Amesema haingii akilini kuona
mizigo inayotoka au kwenda Zanzibar kutozwa kodi baada ya masaa huku
inayotoka nje ya Tanzania ikitozwa baada ya siku saba.
Kuhusu ujio wa Naibu mtendaji Mkuu
mpya Mbarawa aliitaka Bodi na menejimenti kumpa ushirikiano ili aweze
kutoa matokeo chanya kwenye bandari.
“Tunaleta Naibu Mtendaji Mkuu mpya
ambaye atasimamia operesheni, naomba apewe ushirikiano ili kusaidia
Serikali huyu ambaye anakaimu tunamuondoa ameshindwa kwenda na kasi
yetu,” amefafanua Profesa Mbarawa.
Akizungumza baada ya ziara hiyo
Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Ignas Rugaratuka, amesema wamejipanga
kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaitendea haki nafasi waliyopewa kwa
kusimamia mabadiliko ndani ya bandari.
Amesema tangu waingie wamekuwa
wakipambana kuhakikisha kuwa mapungufu ya TPA yanaisha ambapo
wamefanikiwa kurekebisha kwenye utawala kwa kutoa mafunzo kwa watumishi
na kuzuia wizi ambao ulikuwa umekithiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema kuwa tangu aingie katika
mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kurekebisha mapungufu na
kumuahidi waziri kuwa ataongeza jitihada zaidi.
“Kama ni mabadiliko tumefanya
makubwa sana hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika
sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” amesema Mkurugenzi Mkuu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment