Mama Judy Shore
kutoka Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto
(Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel akielezea jinsi Taasisi hiyo
inavyotoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto na mafunzo kwa wafanyakazi wa
kada ya afya hapa nchini katika mkutano na waandishi wa habari uliozungumzia
kambi ya matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua (Catheterization) inayoendelea
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo hadi sasa jumla ya watoto
20 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri.Kulia
ni Daktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo
kutoka JKCI Peter Kisenge.
Daktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter
Kisenge akiongea na waandishi wa Habari kuhusu uhusiano wa Taasisi hiyo na
Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart- SACH) ya nchini Israel
ambapo hadi sasa jumla ya watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo bure nchini
Israel. Kulia ni Simon Fisher na kushoto ni Mama Judy Shore wote kutoka SACH.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto
kutoka Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto
(Save a Child’s Heart - SACH) ya nchini Israel Katharina Schmitt akiangali
jinsi moyo wa mtoto unavyofanya kazi (Echocardiogram)
kwenye kambi ya matibabu na upimaji wa moyo kwa watoto inayoendelea katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Kulia ni Afisa Muuguzi wa JKCI Pal
Bhadreshwara na kushoto ni mama wa mtoto.
Watoto wakicheza wakati wakisubiri kwenda kufanyiwa kipimo
kinachoangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram) katika kambi ya matibabu ya moyo kwa
watoto inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s
Heart-SACH) ya nchini Israel. Jumla ya watoto 100 wanatarajiwa kufanyiwa
uchunguzi kati ya hao 60 ambao watakuwa na matatizo makubwa watapelekwa
nchini Israel kwa ajili ya matibabu na 40 watatibiwa hapa nchini.(PICHA NA JKCI)
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) ya
nchini Israel wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization)
kwa watoto 20 wenye matatizo ya Moyo.
Upasuaji huo ambao unatumia mtambo wa...
Cathlab umefanyika katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza tarehe 23/11/2017
na kumalizika kesho tarehe 27/11/2017. Matibabu yaliyofanyika ni ya kuziba
matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya moyo.
Katika kambi hii tunatarajia kufanya
uchunguzi wa moyo kwa watoto 100 kati ya hao watoto 60 ambao watakuwa na
matatizo makubwa watapelekwa nchini Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa
kufungua kifua mwakani na watoto 40 watatibiwa hapa nchini.
Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 25
tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata
matibabu. Watoto 20 waliopata matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali
zao zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika.
Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child
Heart- SACH) ya nchini Israel ambapo hadi sasa jumla ya watoto 40 wamefanyiwa
upasuaji wa moyo nchini Israel. Gharama za matibabu ya watoto hawa
zinagharamiwa na Taasisi hii.
Tunawashukuru sana wenzetu hawa wa SACH
kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu bure kwa watoto wenye matatizo ya
moyo. Watoto waliotibiwa wamepona na wale ambao walikuwa wanafunzi
wanaendelea na masomo yao.
Wakati kambi hii inaendelea baadhi
ya wafanyakazi wa SACH na JKCI walienda mkoani Kagera kufuatilia maendeleo ya
mtoto Julius Kaijage (12) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi
Green Acres iliyoko Bunazi ambaye alifanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel
mwaka 2013. Tumekuwa na tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto tunaowafanyia
upasuaji hii inatusaidia sana kufahamu maendeleo yao.
Aidha tunatarajia kuwa na kambi nyingine
ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima
itakayoanza kesho tarehe 27/11/2017 hadi tarehe 01/12/2017. Katika kambi hii
ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya Open Heart International ya
nchini Australia tunatarajia kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa watoto 13
na watu wazima 10.
Tunawaomba wananchi waendeleee kuchangia
damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa
damu wakati wanapatiwa matibabu. Kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha
watu wanaopenda kuchangia damu tunawaomba wafike Taasisi ya Moyo
iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa maelezo zaidi wawasiliane kwa
simu namba 022-2151379 au 0713304149.
Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi
tunaendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya
afya ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na
kuhitaji kupata matibabu.
Kwa namna ya kipekee Bodi ya Udhamini, Uongozi na Wafanyakazi wote
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tunamshukuru sana Mhe. Rais John Pombe
Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 25/11/2017 wakati wa ufunguzi wa
Hospitali ya Taaluma na Tiba ya chuo kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi
Muhimbili kampasi ya Mloganzila kwa kutupatia jengo ambalo tutalifanya
kuwa jengo la watoto.
Kama mnavyofahamu asilimia 70 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji
wa kufungua kifua ni watoto, tuna jumla ya vitanda 123 kati ya hivi
vitanda vya watoto ni 24 tu.
Kuwa na jengo la watoto kutasaidia watoto kupata sehemu
nzuri ya matibabu pamoja na sehemu ya kujifunza mambo mbalimbali kwani watoto
wanahitaji kucheza na kujifunza. Watoto wengine wanakaa wodini muda mrefu
wakisubiri matibabu, watoto hawa wakiwa na mahali pa kujifunzia wataweza
hata kujifunza kusoma na kuandika.





No comments :
Post a Comment