Thursday, November 16, 2017

Ujue mkopo wa “jipange kimaisha na PSPF.”



Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Adam Mayingu, akimkabidhi Baturi Msusi kadi yake ya uanachama wa PSPF itakayomwezesha hata kupata fursa ya kupewa mkopo wa kuanzia maisha mpango unaojulikana kama jipanga kimaisha na PSPF.

Na CHRISTIAN GAYA

Idadi kubwa ya waajiriwa wapya hutumia mapato yao yanayotokana na malipo ya mishahara ya mwisho wa mwezi kuimarisha kujipanga kimaisha ambapo mishahara hiyo haitoshi kuwawezesha kumudu gharama kama kulipa kodi ya nyumba au kununua samani.

Waajiriwa wapya hasa wakiwa ni vijana wamekuwa wakipata ugumu wa kupata kipato cha kuanzia maisha ili kujipanga vizuri kimaisha. Karibu idadi kubwa ya wafanyakazi hapa nchini wote wamepitia hali hii na kukumbuka walivyoanza kazi na kuhitajika kwa mahitaji kadhaa, lakini walikwamishwa na kipato.
Mishahara ya waajiriwa wapya tu mara nyingi haiwezi kukidhi mahitaji yao ya lazima kimaisha kama vile kununua samani za ndani, kulipa kodi ya nyumba, kununua chombo cha usafiri, kugharamia vyombo vya ndoa na harusi. Matokeo yake waajiriwa wapya wengi wameishi kwa kuunga unga tu bila ya kuwa na vyanzo vya fedha vyenye uhakika na hivyo bila kukidhi matakwa yao mapya ya ajira.
Kwa kutambua hili PSPF wameanzisha huduma ya mkopo wa wanachama wapya unaomwezesha mwanachama mpya mchangiaji wa PSPF kujipanga kimaisha.
Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Adam Mayingu anasema mpango  wa mkopo wa kuanzia maisha wa mfuko wa PSPF unaojulikana kama “Jipange Kimaisha" mkopo kwa mwajiriwa mpya umelenga kumwezesha kumudu gharama za mahitaji muhimu ili kukidhi matakwa halisi ya maisha ya waajiriwa wapya ambao ni mwanachama wachangiaji wa mfuko wa PSPF.
Lengo kubwa la mfuko wa PSPF kuanzisha mkopo huu wa kuanzia maisha ni kuhakikisha ya kuwa kila mtanzania anatimiza ndoto yake kwa kupitia mkopo wa kuanzia maisha. Kabla ya mpango huu wa mkopo wa kuanzia maisha, waajiriwa wapya walikuwa hawana fursa ya kupewa mikopo kutokana na taasisi za fedha kuwa na hofu ya usalama wa mikopo yenyewe .
"Hivi ndivyo PSPF ilivyojipanga kwa kuanzisha huduma ya mkopo wa wanachama wapya unaomwezesha mwanachama mpya kujipanga kimaisha kwa kumudu gharama za maisha na kuwa msaada mkubwa sana kwa vijana wengine wakaoingia katika ajira," mkurugenzi mkuu anasema.
Anasema waajiriwa wapya wengi wameanza kunufaika na huduma hii, na wameanza kupeleka taarifa kwa waajiriwa wapya, hasa walioko vijijini na nje ya nchi ambao taarifa za aina hii kwao hawajazipata kwa wakati unaotakiwa na kuhakikisha ya kuwa mpango huu wa mkopo wa kuanzia maisha unawanufaisha idadi kubwa ya wanachama wapya wa PSPF nchini.
"Madhumuni ya kuanzisha mpango huu wa jipange kimaisha na PSPF ni kuwajali wanachama wetu hata wakiwa katika mwanzo wao wa ajira na hiyo inakwenda sambamba na kaulimbiu yetu ya PSPF tulizo la wastaafu" Mayingu anasema.
Anasema mwajiriwa mpya ambaye atajisajiri kuwa mwanachama mchangiaji wa PSPF atastahili kupata mkopo huu wa kujipanga kimaisha baada ya kuchangia kwenye mfuko wa PSPF kwa kipindi cha miezi isiyopungua sita.
"Mwanachama huyo mpya atakayejiunga na PSPF anaweza kukopa hadi kufikia mishahara ya miezi miwili; mfano: kama mwanachama mshahara wake kwa mwezi ni shilingi milioni 1,000,000/ ina maana anaweza kupata mkopo wa kuanzia maisha wa shilingi milioni 2,000,000 za kitanzania kwa mkupuo na huku akilipa taratibu,"anafafanua zaidi.
Anaeleza ya kwamba huduma ya kuanzia maisha ni huduma muhimu sana kwa vijana kwani upataji wa fedha za kujiendeleza kwa kundi hili imekuwa changamoto kubwa hivyo kupatikana kwake imeanza kufungua milango kwa vijana kujimudu gharama za kulipa kodi ya nyumba, kununua samani za ndani, kugharamia ndoa na harusi, kununua chombo cha usafiri n.k. bila vikwazo.
Hivyo natoa wito kwa watanzania wenzetu kujiunga na mfuko wa pensheni wa PSPF ili waweze kufaidika na fursa hii,” Mayingu anasisitiza.
Mwandishi wa makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog   +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment