Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu
Mstaafu, Mizengo Pinda, baada ya kuwasili kwenye Mahafali ya 33 ya Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania mjini Singida ambapo alikuwa mgeni rasmi,
Novemba 30, 2017.
………………
SERIKALI haijatoa ruhusa kwa
Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo
imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Baadhi ya mitandao ilitoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: “Waziri Mkuu aruhusu kozi za ‘Foundation’ Chuo Kikuu Huria”
kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017)
wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali
ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.
Akizungumza na mamia ya wakazi
wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida,
Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanyia maboresho Sera ya Elimu na
Mafunzo ya 2014.
“Kwa sasa Serikali inafanya
maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera tuliyonayo haifafanui
vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa
elimu huria na masafa,” alisema.
“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation,
zinahitaji pia kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu
wetu wanaendelea kuiboresha. Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa
kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote
ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” alisema.
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda alisema wamepokea
barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu
ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi za Foundation katika chuo hicho.
“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation
ulioboreshwa ili kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
na tunasubiri mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema
mwezi ujao,” alisema Prof. Bisanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, DESEMBA MOSI, 2017
No comments :
Post a Comment