Thursday, November 23, 2017

NSSF na tuzo ya kimataifa ya huduma bora

The NSSF Director-General, Prof Godius

Mkurugenzi Mkuu wa  NSSF Prof. Godius Kahyarara

Na CHRISTIAN GAYA

Utoaji wa huduma bora zenye viwango kwa wateja umewezesha Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutunukiwa cheti cha ithibati cha Shirika la Kimataifa la Viwango yaani ISO na uzinduzi ulifanyika, 2014 AICC Arusha.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof Godius Kahyarara anasema tuzo hiyo ilitolewa baada ya ukaguzi wa mahesabu uliofanyika na kubainika shirika hilo la NSSF kuwa na rekodi nzuri na kukidhi viwango vya ubora wa huduma vya kimataifa  yaani ISO 9001, 2008 QMS.
Prof  anasema cheti hicho cha idhibati cha ISO kilitolewa na Taasisi ya Viwango ya  Uingereza cha yaani BSI baada ya kujiridhisha ya kuwa NSSF inatoa huduma bora nchini Tanzania. Anaeleza ya kuwa BSI ni mwanachama wa ISO na sekretarieti ya ISO iko huko Geneva. “Huu ni mtandao wa taasisi za kitaifa za viwango unaojumuisha nchi 161 duniani na taasisi za kiufundi zipatazo 3,368 zinazoratibu maendeleo ya viwango.” anasema.
Mkurugenzi anabainisha ya kuwa ili kukidhi viwango vya kimataifa vya ISO, inabidi kutoa huduma bora, salama na zinazoaminika. Shirika au kampuni inayokidhi viwango hivi inapunguza matumizi kwa kupunguza kasoro katika mifumo ya utendaji na kuongeza tija kazini. Kwa kutekeleza viwango vya ISO 9001, 2008, QMS NSSF imeamua kwa dhati kuendeleza kuboresha huduma zake ili kukidhi matarajio ya wateja wake Prof Kahyarara anaeleza.
Mkurugenzi mkuu anasema kwamba, uongozi wa NSSF umejikita sana kwenye thamani ya biashara kwa wateja wake “ili kujua mahitaji yao kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuwahudumia vizuri zaidi na hali hii inatuwezesha kujua wapi tunafanya vizuri na wapi kuna changamoto bado ili tuweze kujipanga vizuri”
Anasema wateja ndiyo wenye uwezo wa kutathmini vizuri zaidi huduma zao na kuwapa mrejesho sahihi juu ya mambo yanayohotajika kuboreshwa ili kukidhi matarajio yao. “ISO inataka kuona moyo wa  dhati wa kujituma kama ambavyo tumefanya, na ubora wa huduma unatafisiriwa kwa kuwa na tija na moyo wa kuleta mabadiliko chanya katika mifumo mbalimbali ya utendaji ndani ya NSSF. “ Anasisitiza Mkurugenzi mkuu.
Kukabiliana na majanga ambao ni mchakato endelevu na uboreshaji wa mazingira kazini na huduma kwa wateja, alisema kunalenga kutoa kinga ya majanga ya kijamii na kuongeza thamani kwa NSSF.
Prof Kahyarara anasema ubora wa huduma unahusisha uwekezaji wenye tija, mazingira mazuri ya wafanyakazi na kuboresha mafao ya wanachama.  Njia ambayo NSSF  inatumia kutoa kinga dhidi ya majanga ya jamii ni kubaini vyanzo  au dalili zake  kukabiliana na matatizo yanayojitokeza na kuondoa au kupunguza uwezekano wake wa kutokea.
 “Tumekuboreshea huduma zetu na tunataka kuendeleza kutoa huduma bora kwa viwango vya kimataifa  kama ambavyo tumeweza kufikia, tunahakikisha tunaendeleza kutoa huduma bora kwa wakati kwa wateja wetu wote na tunataka kuhakikisha hakuna mteja anayeweza kuchelewa kwenye ofisi zetu kwa zaidi ya saa moja, na kwa sasa tunatoa huduma kwa haraka, kwa ufanisi wa hali ya juu na kujali wateja wetu ndio maana tumeweza kupata cheti hiki cha idhibati cha ISO , hivyo unaweza kuona ni kwa namna gani tumeboresha huduma zetu.” Prof Kahyarara anasisitiza.
Mkurugenzi mkuu anasema kuanzia sasa wanataka mwanachama anayefika kwenye ofisi za NSSF kuomba taarifa za mafao yake ahudumiwe haraka iwezekanavyo kuliko ilivyokuwa zamani  na kwamba ilichukua muda mrefu kutokana na uhaba wa vitendea kazi, teknolojia ndogo na uchanga wa shirika.
Prof Kahyarara anabainisha ya kuwa hata hivyo, cheti cha ISO siyo tu kwamba ni baraka kwao, pia kinawapa changamoto kubwa kuweza kuendelea kutoa huduma bora na kwa wakati.
"Hii ina maana ya kuwa kila baada ya miaka mitatu tutafanyiwa tathmini tena kuona kama bado tunatoa huduma bora. Ofisi zote za mikoa zimesajiliwa na zinapimwa kwa mujibu wa viwango vya ISO 9001:2008." anasema.


Mwandishi wa makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu  +255 655 13 13 41



No comments :

Post a Comment