
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Maadhimisho ya Sherehe za miaka 56
ya Uhuru wa Tanzania Bara yatapambwa na Gwaride la Mkoloni, Makomandoo
na Gwaride la kimyakimya ambapo Rais Magufuli anatarajiwa kuwa Mgeni
Rasmi.
Hayo yameelezwa jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama katika
mahojiano maalum na mwandishi wa habri hii.
Mhe. Mhagama alisema kuwa
maadhimisho ya...
miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatafanyika kitaifa
mjini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi, katika Uwanja wa Jamhuri.
Shughuli zitazofanyika siku hiyo
ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama
vikiwemo jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT), Polisi na Magereza, onesho la gwaride ya mkoloni, kwata ya
kimyakimya na onesho la kikosi cha makomandoo.
Aidha, Mhe. Mhagama alisema kuwa
kutakuwepo burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka Ruvuma, Kigoma
na Zanzibar, kwaya kutoka Chunya, Mbeya na burudani ya muziki kutoka
kikundi cha Tanzania Allstars ikiwemo mziki wa kizazi kipya.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni
“Uhuru wetu ni Tunu: Tuudumishe, Tulinde Raslimali zetu, Tuwe Wazalendo,
Tukemee Rushwa na Uzembe”.
Mhe. Mhagama amezidi kumpongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kulinda rasilimali za nchi hasa madini.
“Vita ya kulinda rasilimali zetu iwe endelevu na ya kila mtu ili rasilimali hizo zimnufaishe kila mtanzania,” alisema Mhagama.
Aliwaomba wananchi wa mikoa ya
Singida, Manyara, Morogoro, Dodoma na watanzania wote kwa ujumla
kujitokeza kwa wingi katika Maadhimisho hayo ya kihistoria ambayo
yataanza saa 12.00 asubuhi mjini Dodoma.
Ni mwaka wa 56 wa luadhimisha
uhuru wa Tanzania Bara ambao ulikomesha utawala wa kikoloni wa
Waingereza, uliopatikana Desemba 9, 1961 chini ya uongozishupavu wa
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
No comments :
Post a Comment