Mtendaji
Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale akionyesha Tuzo ya Rais wa JICA
katika hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam.
Kutoka kulia ni Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshinda, Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, Makamu wa Rais wa JICA
Hiroshi Kato na Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini Tanzania Toshio Nagase.
NA
ISMAIL NGAYONGA MAELEZO
SERIKALI ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa
la nchi hiyo (JICA) imesema itaendelea kuisadia miradi mikubwa ya maendeleo nchini
ikiwemo barabara ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua kubwa katika
kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Hayo
yamesemwa mwishoni wa wiki Jijini Dar es Salaam na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida
wakati wa utoaji tuzo ya heshima ya Rais wa JICA kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD), Mhandisi Patrick Mfugale.
Balozi
Yoshida alisema tangu mwaka 1980, JICA imekuwa mshirika wa karibu wa maendeleo na
Serikali ya Tanzania ikiwemo kuunga mkono juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umasikini
kwa wananchi kupitia ufadhili wa miradi ya kipaumbele kwa ikiwemo barabara.
Aliongeza kuwa utoaji wa
Tuzo ya Rais wa JICA kwa Mhandisi Mfugale imedhirisha imani ya Serikali ya
Japan kwa Tanzania katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
inayofadhiliwa JICA, na kuahidi kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano
huo kwa manufaa ya wananchi wa Mataifa hayo.
“Misaada
ya JICA nchini unajumuisha misaada bila masharti, misaada ya kiufundi,
kufadhili miradi kwenye maeneo ya vipaumbele kwa serikali hususan katika sekta
za kilimo, miundombinu ya barabara, maji, nishati, utawala na afya” alisema
Balozi Yoshida.
Akizungumzia
kuhusu tuzo ya Rais wa JICA kwa Mhandisi Mfugale, Balozi Yoshida alisema tuzo
hiyo hutolewa kama alama ya utambuzi wa heshima kwa wataalamu, wataalamu
washauri na wafanyakazi wa kujitolea walifanikisha maendeleo katika nyanja za
raslimali watu na maendeleo ya miundombinu katika nchi zinazoendelea ikiwemo
Tanzania.
Balozi
Yoshida alisema tuzo hiyo imetolewa kwa Mhandisi Mfugale kutokana na mchango
wake katika maendeleo ya miundombinu inayounganisha mikoa mbalimbali nchini
pamoja na nchi jirani na kueneza ujuzi wake kwa wasaidizi waliomzunguka.
Kwa
upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema
tuzo ya Mhandisi Mfugale imetoa somo kwa Wahandisi vijana wanaopaswa kuzingatia
miiko inayoongoza taaluma ya uhandisi nchini.
Aidha
Prof. Mbarawa aliishukuru JICA kwa utekelezaji wa miradi ya barabara nchini
hususani katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia uchumi wa
kati kupitia uimarishaji wa miundombinu imara ya barabara.
“Uadilifu
na uaminifu ni jambo la msingi sana katika taaluma ya uhandisi, ni misingi
mikuu iliyoonyeshwa katika utendaji kazi Mhandisi Mfugale hadi anatunukiwa tuzo
hii, niwahimize wahandisi vijana muige mfano huu” alisema Waziri Mbarawa.
Naye
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), Mhandisi Patrick
Mfugale alisema tuzo aliyopewa ni zawadi kwa Serikali hususani wafanyakazi wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambao amekuwa akifanya nao kazi kwa katika kutekeleza majukumu yake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akimpongeza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patric Mfugale
kwa kupewa Tuzo ya Rais wa JICA mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam. Tuzo
hiyo imetolewa kwa watu binafsi 23 dunia ikiwa ni kutambua michango yao katika
kusimamia miradi ya JICA.
Baadhi
ya wafanyakazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) na Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS) wakifutilia hafla ya kumkabidhi Tuzo ya Rais wa
JICA Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale mapema wikiendi hii. Tuzo
hiyo imetolewa kwa watu binafsi 23 dunia ikiwa ni kutambua michango yao katika
kusimamia miradi ya JICA.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale akipokea shada la maua kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wenzake Bi. Beatrice Kosongwa wakati wa hafla ya kumkabidhi Tuzo ya Rais wa JICA iliyofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshinda, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, Makamu wa Rais wa JICA Hiroshi Kato na Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini Tanzania Toshio Nagase.(PICHA NA: FRANK SHIJA – MAELEZO





No comments :
Post a Comment