Balozi wa India nchini Tanzania
Bw. Sandeep Arya, akieleza nia ya nchi yake kuwekeza katika Sekta ya
Nishati, Kilimo, Ujenzi wa Mji wa Dodoma na miundombinu mingine kama
Reli na Barabara wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) na Kamishna Msaidizi wa Sera, Bi
Sauda Msemo wakimsikiliza kwa makini Balozi wa India nchini Tanzania Bw.
Sandeep Arya akielezea jitihada za nchi yake katika kuwekeza kwenye
masuala ya Afya wakati wa mkutano kati ya pande hizo mbili Jijini Dar
es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tatu kushoto) na Maafisa waandamizi wa
Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa makini maelezo ya Balozi wa
India nchini Tanzania Bw. Sandeep Arya (hayupo pichani) kuhusu utayari
wa kuwekeza katika Sekta ya Umeme hasa umeme wa Jua, wakati wa Mkutano
kati ya pande hizo mbili Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa India nchini Tanzania
Bw. Sandeep Arya (kulia) akielezea kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati
ya nchi hizo mbili hasa katika masuala ya kibiashara wakati wa Mkutano
kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb) (wa tatu kulia), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha Jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wa pili kulia akielezea kuhusu uwekezaji
wenye kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ambao ni fursa kwa nchi hiyo,
wakati wa Mkutano na Balozi wa India nchini Tanzania Bw. Sandeep Arya
(wa pili kulia), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar
es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiagana na Balozi wa India
nchini Tanzania Bw. Sandeep Arya, baada ya kumalizika kwa mkutano kati
yao Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kulia), Balozi wa India nchini
Tanzania Bw. Sandeep Arya, Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na
Mipango na Ubalozi wa India wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya
kumalizika kwa mkutano ulioangazia Uwekezaji na biashara, Jijini Dar es
Salaam.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango
………………
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Serikali ya India imeahidi kutoa
mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza
mradi mkubwa wa maji katika miji 17 nchini kupitia Benki ya Exim ya
nchini humo.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India hapa nchini Bw.
Sandeep Arya.
Dkt. Mpango alieleza kuwa mradi
huo umelenga kumtua ndoo mama kichwani na kwamba mkopo huo utakapo
patikana utasaidia kutatua kero kubwa ya maji inayoikabili jamii hivyo
kuchochea kwa kasi ukuaji wa uchumi.
“Tuko katika mazungumzo ya
kukamilisha upatikanaji wa mkopo huo ikiwemo kuangalia namna ya
kushughulikia madai ya Benki ya Exim ambayo inataka hata kampuni
itakayotekeleza mradi huo isamehewe kodi zote zikiwemo zinazopaswa
kulipwa na wafanyakazi wake” alieleza Dkt. Mpango
Alibainisha kuwa licha ya kwamba
jambo hilo ni gumu kisheria lakini kutokana na umuhimu wa suala hilo la
maji, Serikali italipatia ufumbuzi hivi karibuni ili mradi huo uweze
kuanza mara moja.
Dkt. Mpango alitambua mchango
mkubwa wa Serikali ya India katika kutatua changamoto ya maji kwa
watanzania ambapo amesema kuwa inchi hiyo inatatekeleza mradi mkubwa wa
maji wa Ziwa Victoria-Shinyanga hadi Tabora.
Dkt. Mpango aliiomba Serikali ya
India iendelee kuisaidia Tanzania katika Nyanja za utaalamu wa
teknolojia ya habari na mawasiliano-TEHAMA ili kupata watu wenye ujuzi
utakao saidia kuchochea kasi ya maendeleo ya Sekta ya Viwanda nchini.
Dkt. Mpango alisema kuwa nchi ya
India imepiga hatua kubwa katika masuala ya TEHEMA hivyo ni vema
ikawekeza kwenye eneo hilo katika Taasisi za Elimu hapa nchini ili
kuweza kuwapatia ujuzi idadi kubwa ya watu watakao kwenda kusukuma
gurudumu la maendeleo hasa ya ukuaji wa viwanda.
“Bila kuwa na watu wenye ujuzi
katika kada mbalimbali hasa TEHAMA hatuwezi kuwa na nchi yenye uchumi wa
viwanda”, aliongeza Dkt. Mpango.
Aliyataja maeneo yenye fursa
kubwa za uwekezaji kuwa ni pamoja na Sekta ya Kilimo ambapo Tanzania
inahitaji kuwa na viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao na pia kuwa
na zana bora za kilimo kama utumiaji wa Trekta badala ya kutumia jembe
la mkono.
Maeneo mengine ni sekta ya utalii,
afya, uendelezaji wa ujuzi kupitia fani nyeti za udaktari ama utaalamu
nyeti ya tiba ikiwemo magonjwa ya moyo na figo, ambayo India imepiga
hatua kubwa.
“Pia ujuzi wa Wahandisi katika
Sekta ya Maji unahitajika ili kutoa huduma ya maji kwa weledi kwa jamii
kwa kuwa ni moja ya hitaji muhimu kwa maendeleo, hata hivyo zipo sekta
nyingine za uwekezaji kama Utalii na Uvuvi hasa katika kina kirefu
ambao unahitaji zana bora” aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake Balozi wa India
nchini Tanzania Bw. Sandeep Arya, amesema nchi yake inania ya kuwekeza
katika Kilimo, Nishati ya Umeme hasa wa Jua na kusaidia katika mpango wa
ujenzi wa Mji wa Dodoma pamoja na ujenzi wa Reli na Barabara.
Amesema Tanzania na India
zinauhusiano wa muda mrefu hivyo nchi yake itaendelea kuwekeza Tanzania
katika Nyanja mbalimbali ili kuendeleza ushirikiano wenye tija kwa
wananchi wa pande hizo mbili.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), amemshukuru Balozi wa India na Nchi yake
kwa nia ya kuendelea kuwekeza Tanzania na kusifu juhudi za uwekezaji
mkubwa ambao unafanywa hasa katika Sekta ya Afya na kuahidi kuendelea
kudumisha ushirikiano huo
No comments :
Post a Comment