Mkurugenzi wa Shughuli za Takwimu
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw, Irenius Ruyobya akizungumza
na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika
inayotarajiwa kuadhimisha tarehe 20 Novemba jijini Dar es Salaam. Kulia
ni Mtakwimu Mwandamizi wa ofisi hiyo Bw. Philemon Mwenda.
Waandishi wa Habari wakifuatilia
mkutano wa Mkurugenzi wa Shughuli za Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) Bw, Irenius Ruyobya alipokuwa akizungumza kuhusu
maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika inayotarajiwa kuadhimisha tarehe
2o Novemba jijini Dar es Salaam.
Picha na MAELEZO
……………
Na: Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam
Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya
Takwimu Afrika yatakayofanyika tarehe 20 Novemba, 2017 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya amesema...
maadhimisho hayo yanayoratibiwa na ofisi hiyo kwa niaba ya Serikali,
yana lengo la kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa Tasnia ya
Takwimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii Barani Afrika.
Ruyobya amesema kuwa kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka huu ni “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora”
“Kaulimbiu hii inalenga kuweka
mkazo katika matumizi ya Takwimu za Uchumi kwa ajili ya kuboresha
maisha ya wananchi wote nchini na Afrika kwa ujumla”, amebainisha
Ruyobya.
Ruyobya amefafanua kuwa
matumizi sahihi ya Takwimu za Uchumi yanaiwezesha Serikali kutunga sera
na kutathmini programu mbalimbali kama vile Mpango wa Taifa wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (FYDP-II), Agenda ya Dunia ya Mwaka 2030 ya Malengo ya
Maendeleo Endelevu (SDGs) na Agenda ya Afrika ya Mwaka 2063.
“Progaramu zote hizi, zina
lengo la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa, kuna
upatikanaji wa Huduma za afya, Elimu,
Miundombinu ya umeme na barabara, Mawasiliano, Utunzaji wa mazingira pamoja na Utawala bora”, amesema Ruyobya.
Jumla ya washiriki 200 kutoka
katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Vyuo
vya Elimu ya Juu, Wanafunzi wa Shule za Sekondari pamoja na Wadau
mbalimbali wa takwimu nchini wanatarajiwa kuhudhuria kwenye maadhimisho
hayo.
Tarehe 18 Novemba ya kila
Mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine Barani Afrika kuadhimisha Siku
ya Takwimu Afrika, kutokana na siku hii kuwa Jumamosi, maadhimisho
haya yatafanyika Jumatatu tarehe 20 Novemba, 2017.
No comments :
Post a Comment