Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk.Binilith Mahenge
…………….
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Binilith Mahenge amezitaka Halmashauri za Wilaya, Mji na Manispaa Mkoani
Dodoma kuhakikisha zinatenga asilimia kumi (10%) ya makusanyo yao ya
ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na Walemavu kuanzisha miradi ya
viwanda vidogo na vya kati.
Lengo ni kuitikia kampeni ya
Serikali inayoitaka Mikoa kuanzisha viwanda kama ilivyozinduliwa hivi
karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Seleman
Jafo.
Akizungumzia hilo, ameonya tabia
ya baadhi ya Halmashauri kutotoa asilimia kumi (10%) ya makusanyo yake
ya ndani au kutoa kiasi kidogo kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu
na kuwa utaratibu unaotumika sasa wa Halmashauri kukopesha fedha hizo
wakati mwingine sio muafaka sana badala yake Halmashauri zitumie fedha
hizo kuwafungulia vijana, wanawake na walemavu viwanda vidogovidogo na
kuwakabidhi waendeleze uzalishaji na kuviendesha.
Dkt. Mahenge amebainisha hayo
wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Wilaya za Mkoa wa
Dodoma kujitambulisha na kukagua miradi ya maendeleo ambapo amesema kuwa
viwanda vinavyoweza kuanzishwa ni vya uchakataji wa nafaka, usindikaji
mazao na utengenezaji vyakula vya Mifugo.
Amesema kuwa asilimia kumi hiyo
ikitumika na kusimamiwa vizuri inaweza kutekeleza kampeni ya kuanzisha
viwanda ambapo vijana na wanawake wanaweza kufaidika kuanzia ngazi za
chini kama vijijini kwa kupata ajira kipato na halmashauri kupata
ushuru.
Aidha, ameongeza kuwa mbali na
uanzishaji viwanda miradi mingine Halmashauri inayoweza kuwaanzishia
vijana, wanawake na walemavu ni pamoja na ufugaji samaki kwa kuwachimbia
mabwawa.
Ametaja miradi mingine mbali na
viwanda kuwa Halmashauri zinaweza kuchimba visima na kujenga miundombinu
ya umwagiliaji ili vijana, wanawake na walemavu waendeshe kilimo cha
umwagiliaji kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yanaweza kuwa malighafi
kwenye viwanda vinavyoanzishwa.
“Sisi ni Viongozi, maana ya kuwa
viongozi ni pamoja na kuwasaidia wananchi kuweza kufanya maamuzi yenye
manufaa kwao na uanzishwaji wa viwanda utawanufaisha wananchi wengi na
Mkoa kwa ujumla” alimalizia Dkt. Mahenge.