Friday, November 10, 2017

BEI YA KOROSHO YAPANDA PWANI ,YAUZWA SH.3,817 KWA KILO

IMG-20171109-WA0056
Baadhi ya wanunuzi wa korosho wakiwa wanasubiri uzinduzi wa mnada wa kwanza wa korosho mkoani Pwani ,uliofanyika wilayani Kibiti
IMG-20171109-WA0053
Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo wa kwanza kulia akitoka kuangalia ghala la korosho huku akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Kibiti, Gulamhussein Kifu siku ya uzinduzi wa mnada wa kwanza wa korosho Mkoani hapo uliofanyika Kibiti
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti
MNADA wa kwanza wa ununuzi wa korosho ,mkoani Pwani uliofanyika wilayani Kibiti ,umefanikiwa kuuza korosho daraja ya kwanza kwa bei ya sh. 3,817 kwa kilo huku daraja la pili ikinunuliwa kwa sh .2,950.
Bei hiyo imeongeza katika msimu huu tofauti na msimu ...
wa mwaka 2015/2016 ambapo korosho daraja la kwanza ilinunuliwa kwa sh.2,900 kwa kilo na daraja la pili sh.2,500.
Licha ya mnada huo kufanikiwa lakini mkoa huo bado unahitaji magunia 200,000 kwa ajili ya kuhifadhia korosho zilizovunwa msimu huu ambazo zinafikia zaidi ya tani 25,000.
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo akizindua mnada huo alieleza msimu huu mavuno yamekuwa ni makubwa na korosho ni nyingi .
Alieleza kutokana na hilo magunia yanahitajika kwa wingi ili kuhifadhi korosho hizo.

Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ,walipatiwa magunia 30,000 ambayo hayakutosheleza kwani yote yameisha na bado kuna mahitaji makubwa licha ya kwamba wamehakikishiwa hivi karibuni yatapelekwa magunia mengine.
Alielezea wilaya ya Kibaha na Kisarawe zilishindwa kufika kwenye mnada huo kutokana na kukosa magunia ya kuhifadhia korosho na mkoa unafanya kila njia kuhakikisha magunia hayo yanapatikana.

“Changamoto hii inabidi tukabiliane nayo kwa kukaa na mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha wawekezaji waje wawekeze kiwanda cha magunia lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo hili,” alisema mhandisi Ndikilo.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulamhussein Kifu alisema ,wakati wanahifadhi korosho ambazo zimenunuliwa wataingia mikataba na vyama vya msingi ambavyo ndiyo wenye korosho ili kusitokee kupungua kwa korosho zilizohifadhiwa.

Alibainisha kumekuwa na changamoto ya kupungua kwa korosho ambazo zimehifadhiwa hivyo kusababisha malalamiko kwa wanunuzi na kwa watakaohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kibiti, Bainga Bwenda alisema, kwenye mnada wa kwanza wamepata kilo milioni 3.8 za daraja la kwanza imezidi minada sita ya mwaka jana kwa kilogramu 100,000.

Anasema kuna mafanikio makubwa yaliyotokana na serikali kutoa pembejeo bure na mfumo wa stakabadhi ghalani lakini changamoto iliyojitojeza ni uhaba wa magunia .

No comments :

Post a Comment