Friday, September 1, 2017

BANDARI KAVU YA KWALA –VIGWAZA KUANZA KUTUMIKA JANUARI MWAKANI.


Waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasilino, Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia ya njano akiwa katika majukumu ya ukaguzi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza inayojengwa mkoani Pwani.


Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA) Eng. Deusdedit Kakoko akifafanua jambo kwa waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasilino, Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu ya Kwala –Vigwaza mkoani Pwani.


NA WUUM, PWANI
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Vigwaza Mkoani Pwani na kumtaka mkandarasi Suma JKT kuongeza kasi na kuzingatia ubora.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanaunganisha kwa haraka ili reli na barabara zinazoingia katika bandari kavu hiyo zinakamilika na hivyo kuiwezesha bandari kavu hiyo kuanza kutumika ifikapo Januari mwakani.
“TPA, TRL na TANROADS uzuri wote mko kwenye wizara moja shirikianeni na hakikisheni kilomita 15 za barabara inayoingia kwenye bandari kavu hii na kilomita moja ya reli zinajengwa haraka,” Amesema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko kuhakikisha ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza unazingatia ubora na viwango vilivyopo katika mkataba ili kuiwezesha kuhudumia zaidi ya makontena milioni moja kwa mwaka na hivyo kupunguza msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Hakikisheni eneo la bandari kavu linakuwa na maegesho ya kutosha, taa, maji ya uhakika, gari la zimamoto, uzio na mashine ya ukaguzi wa mizigo scanner itakayowezesha kupima kila mzigo unaopandishwa na kushushwa katika eneo hili,” amesisitiza Profesa Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Kakoko amesema TPA imejipanga kuhakikisha ujenzi huo unatumia gharama nafuu na mifumo yote ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA inakuwepo katika bandari hiyo ili kuiwezesaha kufanya kazi kisasa na kwa ufanisi zaidi.
“Tukifanikiwa kuhamia hapa mzigo uliokuwa unasafirishwa kwa siku saba sasa utatumia siku tatu kufika Mwanza hali itakayovutia wasafirishaji wengi kutumia bandari ya Dar es Salaam na hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuibua fursa za ajira,” amesema Eng. Kakoko.
Bandari Kavu ya Kwala –Vigwaza inayojengwa na Mkandarasi SUMA JKT ambapo takribani kiasi cha shilingi bilioni 9 kinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ili kuboresha huduma za usafirishaji katika bandari ya Dar es Saalaam ambapo zaidi ya hekta 500 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo ambapo kwa kuanza hekta 120 sawa asilimia 24 zinajengwa katika awamu ya kwanza.




Waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Eng. Charles Salu Ogare anayesimamia ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza  mkoani Pwani.

No comments :

Post a Comment