Wednesday, August 2, 2017

WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA SOKO LA MUHOGO NCHINI CHINA.


RZ8A0289
Jovina Bujulu-MAELEZO.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za dunia hii imebabarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo zikitumika ipasavyo itaondokana na tatizo la umaskini.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki alipokuwa akizungumzia fursa  za kibiashara zinazoweza kupatikana nchini China na kuinua hali ya uchumi kwa wananchi wa Tanzania.
Balozi Kairuki alisema kuwa ni aibu kwa nchi za Kiafrika ambazo zimepata uhuru kwa... zaidi ya miaka 50 kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hususan nchini China.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba, maji, mito na maziwa hivyo tukitumia rasilimali hizi kwa kuunganisha na nguvukazi, uwezo na mitaji tuliyo nayo tunaweza kabisa kupaisha uchumi wa nchi yetu sisi wenyewe” alisema Balozi Kairuki.
Kwa mujibu wa nyimbo za kujenga uzalendo kwa nchi zinakiri kuwa ni nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka, nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri, nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania. Ni vema kuijenga kuisimamia kwa manufaa ya Watanzania.
Balozi Kairuki alisema kuwa kufuatia kusainiwa kwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na China, mwezi Mei mwaka huu watanzania watapata fursa ya kuuza zao la muhogo mkavu nchini China kwa kiwango kikubwa hatua ambayo itainua hali zao hilo kiuchumi na kuweza kuanzisha viwanda nchini.
“Hii ni fursa, natoa rai kwa Watanzania wenzangu tuichangamkie na tujitokeze kwenye maonesho ya biashara yatakayofanyika nchini China mwezi wa 10 mwaka huu, na kuhakikisha tunapata fursa ya kuona mashine za kuchakata na kulimia ili tuweze kuzinunua na kuzitumia katika uzalishaji  mazao ya muhogo” alisema Balozi Kairuki.
Ili kuhakikisha zao hilo linawanufaisha Watanzania, Balozi Kairuki alisema kuwa ni muhimu kuchangamka fursa hiyo wasije wageni wakiwemo Wakenya na Wachina wakaanza kulima zao hilo na kuwazidi Watanzania ambao ni walengwa wa kupeleka zao hilo nchini China.
Aidha, aliongeza kuwa kuwepo kwa fursa hiyo ni fahari kwa nchi Tanzania hatua ambayo itatoa nafasi katika ngazi mbalimbali kununua mitambo ya kuchakata mazao ya mihogo na kutengeneza bidhaa zitokanazo na muhogo.
Mkataba huo utakuwa ni miaka mitano, Watanzania wanatakiwa kuchangamka mapema ili kufaidi matunda ya uwepo wake kabla hujamalizika kwa namna mbalimbali hata baada ya mkataba huo kuisha. Fursa hiyo inatoa nafasi pia ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao yatokanayo na zao la muhogo na hatimaye kukamata soko la bidhaa hiyo.
China ni nchi ambayo ina mahitaji makubwa ya muhogo ambapo kwa mwaka wanaingiza muhogo wa thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni tano.
Katika bara la Afrika nchi ya Nigeria ndiyo pekee inayouza muhogo China, hivyo Tanzania itakuwa nchi ya pili barani Afrika kuuza muhogo nchini humo.
“Kutokana na  sababu za kijiografia Tanzania inaweza kusafirisha bidhaa hiyo kwa urahisi zaidi kuliko nchi ya Nigeria hivyo ni rahisi kuteka soko la zao hilo nchini China” alisema Balozi Kairuki.
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inatakiwa kueleza taratibu za kufanya na kutoa elimu kwa umma kuelezea taratibu za kufuata kuweza kulima muhogo na kuuza nchini China.
Aidha, wananchi wanatakiwa kulima kilimo  chenye tija  kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuzalisha mihogo yenye ubora na inayokidhi mahitaji ya soko la kimataifa kwa wingi.
Balozi Kairuki alitoa wito kwa wadau wa kilimo ambao ni pamoja na wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na taasisi zilizo chini yake, Halmashauri na vituo vya utafiti wa kilimo kuwasaidia wakulima kutatua changamoto zozote zinazoweza kujitokeza ili waweze kujipatia mazao mengi na kuliteka soko la muhogo nchini China.
Nchi nyingine ambazo zinazouza mazao ya muhogo nchini China ni pamoja na Thailand, Brazil na Indonesia ambayo hutumika kutengeneza madawa, biskuti na kwa ajili ya chakula.

No comments :

Post a Comment