………………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Jumla ya wasichana 3,738 wa Mikoa
ya Mara na Geita wanategemea kunufaika na mradi wa...
Kuzuia Ndoa za
Utotoni na Ukeketaji unaofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na
kuratibiwa na shirika la Plan International kwa kushirikiana na
mashirika ya CDF, NELICO pamoja na Molly”s Network.
Takwimu hizo zimetajwa leo na
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Plan – Tanzania, Gwynneth Wong wakati
wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Umoja wa
Ulaya Jijini Dar es Salaam.
Bi. Gwynneth amesema kuwa mradi
huo ni moja kati ya miradi inayoratibiwa na shirika hilo ikisaidiana na
Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha haki za wasichana zinalindwa na
hakuna msichana atakaeachwa nyuma kwenye nyanja za maendeleo hali
itakayopeleka wasichana kuwa na haki sawa na wavulana.
“Tumeona kuna haja ya kuweka mradi
mwingine utakaodumu kwa miaka mitatu wa uzuiaji wa mimba za utotoni na
ukeketaji kwa mikoa ya Mara na Geita kwani mikoa hiyo imeonekana
kuongoza kwa matatizo hayo hivyo tunaushkuru Umoja wa Nchi za Ulaya kwa
kutoa jumla ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuendeshea mradi
huu,”alisema Bi. Gwynneth.
Bi. Gwynneth ameongeza kuwa
takwimu za mwaka 2016 za Utafiti wa Demographia na Afya unaonyesha kuwa
ndoa za utotoni mkoani Mara ni asilimia 55 na kwa Geita ni asilimia 37
na ukeketaji kwa Mkoa wa Mara ni asilimia 32 kwa asilimia za kitaifa
hivyo ni lazima kuanza na maeneo yaliyoathirika zaidi.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa
Ulaya, Roeland Van de Geer amesema kuwa umoja huo unatambua nafasi ya
msichana katika jamii na nafasi ya baadhi ya mashirika yanayoshirikiana
na Serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuhakikisha haki
sawa kwa wote.
“Sisi tunatoa fedha lakini nyie
ndio watendaji hivyo tunawashukuru sana, lakini pia tunatakiwa tutambue
kuwa maendeleo ya kudumu hayawezi kupatikana kwa kuwaacha wanawake nyuma
kwa maana hiyo tunatakiwa tufanye juhudi za kuhakikisha tunaenda
pamoja,” aliongeza Balozi Roeland Van de Geer.
Pia, Balozi huyo ameyashukuru
baadhi ya mashirika yanayojitolea kufanya kazi ya kuhakikisha haki za
msingi za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa na ametoa wito kwa
mashirika mengine kuendelea kusaidia maendeleo ya wasichana kwa sababu
haki zao ndizo zinazovunjwa zaidi.
Mradi huo una malengo ya
kuhakikisha wasichana wanaweza kuelewa haki zao na kuweza kutoa mawazo
yao kwa jamii, kuhakikisha Serikali inasaidia wasichana kumaliza tatizo
la ndoa za utotoni na ukeketaji.Kwa Mkoa wa Mara mradi utatekelezwa
katika Wilaya ya Tarime ambapo utagusa jumla ya Kata tano na Geita mradi
utagusa Kata 4.
No comments :
Post a Comment