Afisa Lishe kutoka Kitengo cha
Lishe Wizara ya Afya Fatma Ali Said akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu wiki ya unyonyeshaji katika ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja
Mjini Zanzibar.
(Picha na Ramadhani Ali)
………………………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali-Maelezo Zanzibar
Akinamama wamehimizwa kuendelea
kunyonyesha watoto wao maziwa ya kifua pekee katika
kipindi cha miezi
sita ya mwanzo bila ya kuwapa chakula chengine ili kuwajenga katika afya
bora na kukua vizuri kiakili na kimwili.
Afisa Lishe kutoka Kitengo cha
Lishe Wizara ya Afya Fatma Ali Said ameeleza hayo katika ukumbi wa
wizara hiyo Mnazimmoja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji iliyoanza jana.
Alisema maziwa ya mama pekee
katika kipindi cha miezi sita ya mwanzao yanamkinga mtoto na maradhi
mengi kwani yanavirutubisho vya kutosha vya kuwawekea kinga na kujenga
upendo baina yake na mama.
Afisa huyo alisema mama
anaponyonyesha mtoto kipindi hicho bila kumpa kitu chengine inapunguza
kutoka damu nyingi katika siku 40 baada ya kujifungua na humsaidia
kurudi katika hali yake ya kawaida kwa haraka.
Alikumbusha kuwa kunyonyesha
mtoto maziwa ya kifua pekee katika miezi sita ya mwanzo hakuna gharama
kwa wazazi na baadhi ya akinamama inawasaidia kujiepusha na mimba
nyengine katika kipindi hicho na kupelekea uzazi wa mpango.
Alisema bado jamii kubwa ya
Wazanzibari haina mwamko wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee miezi sita
ya mwanzo na utafiti uliofanywa mwaka jana unaonyesha ni asilimia 20
tu ya akinamama ndio wanaonyonyesha kwa kutumia utaratibu huo.
Aliongeza kuwa madai ya baadhi ya
watu kwamba maziwa ya mama pekee bila chakula chengine hayamtoshelezi
mtoto hayana ukweli iwapo mtoto atanyonyeshwa kwa muda unaotakiwa.
Alisema mtoto anatakiwa anyonye
kwa dakika zisizopungua 20 bila kupumzika ili apate maziwa yalioko mbali
ambayo ndio yenye chakula na mafuta kwa ajili ya kumjenga mtoto.
“Maziwa ya mwanzo ya mama
yanamaji mengi lakini maziwa yanayochelewa kwa dakika 20
yanavirutubisho vyote muhimu katika makuzi ya mtoto,” aliongeza Afisa
Lishe.
Aliwataka akinamama
wanaofanyakazi sehemu mbali mbali kufanya juhudi ya kuwakamulia maziwa
watoto wao na kuyahifadhi vizuri ili waweze kupewa wakati hawapo
majumbani.
Aidha aliwakumbusha akinamama
kuendelea kunyonyesha watoto wao iwapo itatokea bahati ya kupata mimba
nyengine wakati mtoto aliezaliwa bado anaumri mdogo kwani maziwa ya mama
mjamzito hayana madhara yoyote kwa mtoto.
Kilele cha wiki ya unyonyeshaji
kitakuwa tarehe 7 mwezi huu katika Wilaya ya Micheweni na kauli mbiu ya
mwaka huu Tudumishe unyonyeshaji kwa pamoja.
No comments :
Post a Comment