Hivi Karibuni, Rais wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kwa
pamoja waliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka
Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania. Katika Makala hii pamoja na
mambo mengine Mwandishi Said Ameir wa Idara ya Habari- MAELEZO anaeleza kwani nini mradi huu ni...
kipimo cha utayari na ujasiri wa watanzania katika kuchangamkia fursa.
Mradi huu unaojulikana kama Mradi
wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)
unatekelezwa kwa ubia kati ya washirika wa sekta binafsi na sekta za
umma za nchi za Tanzania na Uganda.
Washirika hao ni Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Petroli ya
Uganda (UNOC), Kampuni ya Mafuta ya Total ya Ufaransa, Kampuni ya TULLOW
yenye makao makuu yake London nchini Uingereza na Kampuni ya China
National Offshore Oil Company (CNOOC).
Bomba ambalo litagharimu dola za
kimarekani 3.5 bilioni, sehemu yake kubwa yaani kilomita 1,115 kati ya
kilomita 1,445 litajengwa katika ardhi ya Tanzania na kupita mikoa 8,
wilaya 24 na vijiji 184.
Kutokana na hali hiyo, inaelezwa
kuwa, mradi huu wakati wa ujenzi na utakapokamilika, utatoa na fursa
nyingi za kiuchumi ambazo zitasaidia sana kuchangamsha shughuli za
kiuchumi hivyo kuchangia ukuaji uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya
watanzania kwa namna mbalimbali.
Mradi huu ni mfano wa ushirikiano
kati ya nchi za Tanzania na Uganda na kwa upande mwingine ni mfano mzuri
wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma katika nchi
hizi.
Katika hatua mbalimbali za
utekelezaji wake, mradi huu utahitaji ushiriki wa sekta binafsi katika
nchi zote mbili na wakati mwingine hata taasisi nyingine za umma ambazo
zinatoa huduma zitakazohitajika na mradi.
Kwa hiyo, wakati tukisifia kuwa ni
mfano wa mradi wa ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi katika nchi
zetu, watanzania hawana budi kuelewa kuwa wana wajibu mkubwa wa
kuzitumia vyema fursa za mradi huu.
Kwa Tanzania, mradi huu unaweza
kuonesha picha halisi ya ushirikiano wa sekta hizo kwa kuzingatia namna
makampuni na taasisi za humu nchini zitakavyoweza kushiriki na
kufanikisha mradi huu.
Kwa maana nyingie ni mradi ambao
unaweza kutumika kupima utayari, umakini, uwezo na ujasiri wa watanzania
katika kuchangamkia fursa za kiuchumi.
Kama alivyoeleza Rais Magufuli
wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kuwa katika mradi huu,
Serikali imesamehe mambo mengi ili uweze kutekelezwa kwa kuishirikisha
Tanzania. Wataalamu wa nchi walichambua na kupembua hadi kubaini kuwa
kusamehe huko kutafidiwa na fursa nyingi zitakazoletwa na mradi huu.
Kwa maana hiyo bila ya watanzania
kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha wanazitumia kadri
itakavyowezekana fursa hizo uamuzi huo wa Serikali kusamehe hivyo
ilivyovisamehe hautakuwa na maana yeyote.
Kuja kwa mradi huu Tanzania,
watanzania hawana budi kuipongeza Serikali chini ya Rais John Pombe
Magufuli kwa jitihada kubwa kwa kutumia ushawishi wa kisiasa,
kidiplomasia, uchumi na ukaribu wa viongozi wa nchi hizo mbili pamoja na
hoja nyingine hadi kufanikisha mradi huu kuja Tanzania.
Jitihada hizi ni kielelezo cha
dhamira ya kweli iliyonayo Serikali ya Awamu ya Tano ya kutafuta kila
aina ya fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kutimiza ahadi zake kwa
watanzania ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara.
Serikali imejitwika mzigo mkubwa
wa kushiriki katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa aina yake lakini
imefanya hivyo kwa kuamini kuwa watanzania wako tayari na wako imara
kuupokea kwa hali na mali.
Imeelezwa mara kwa mara kuwa mradi
huu utaliingizia taifa mapato makubwa, utaleta tekinolojia na utalaamu
na fursa za kiuchumi ambazo watekelezaji wake kwa kiwango kikubwa ni
kutoka sekta binafsi. Kwa mnasaba huo, Serikali hapa imefanya zaidi ya
wajibu wake ambao ni wa kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji.
Wale wahenga wa Cambrigde walisema“give us the tools and lets finish the job”
na hivi ndivyo ilivyofanya Serikali kwa mradi huu. Imeleta mradi na
kufungua fursa tele ambazo watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga
kiuchumi wao binafsi na uchumi wa taifa.
Haitakuwa na maana hata kidogo
katika ngazi ya serikali na katika ngazi ya Mtanzania mmoja mmoja kufika
wakati fursa za mradi huu kuchukuliwa na wageni kwa sababu zozote na
katika mazingira yeyote yale. Ikifikia hatua hiyo watanzania watakuwa
wamewaangusha viongozi wao.
Hii kutokana na mazingira ambayo
Serikali imeyaweka kuwawezesha watanzania kushiriki katika sekta ya
mafuta na gesi asilia. Mbali ya kupitisha Sheria ya Local Content Act ya 2015
ambayo inasisitiza ushiriki wa watanzania lakini zaidi dhamira ya kweli
ya kisiasa iliyonayo uongozi wa Serikali ya kuhakikisha kuwa watanzania
wanafaidika ipasavyo na mradi huu.
Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa
baadhi ya Taasisi za Serikali na za sekta binafsi zimeshaanza maandalizi
au zimejitokeza kuwaandaa watanzania kuchangamkia fursa hizo na
kuhakikisha wanazitumia vyema.
Miongoni mwa taasisi hizo ni
Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ambayo
inawakusanya pamoja watoa huduma katika sekta hiyo ambapo lengo lake
kubwa ni kuhakikisha kuwa fursa za mradi huo zinatumika ipasavyo kwa
manufaa ya muda mfupo na mrefu ya watanzania.
ATOGS, kama taasisi nyingine
zitakazoelezwa baadae, imeonesha mfano wa utayari kwa kuwa na mpango
mkakati wake ambao unalenga kuwawezesha watoa huduma wa humu nchini
wanapata fursa hizo kwa kuwasaidia kwa namna mbali mbali tangu hatua za
awali za kuwania fursa hizo hadi utekelezaji wake.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo
Abdulsamad Abdulrahim katika moja ya mikutano na waandishi wa habari
alisema taasisi yake imejipanga kuwajengea uwezo watoa huduma na kutoa
wito watoa huduma hao kwa waliokuwa bado hawajajiunga wajiunge na
taasisi hii kwa minajili ya kufaidika na uwezeshaji wao.
Halikadhalika, Baraza la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) nalo linaeleza kuwa limejidhatiti
kuhakikisha kuwa watanzania watakaobahatika kupata fursa za kutoa huduma
katika mradi huo hawashindwi kwa kukosa fedha za kutekeleza kandarasi
zao.
“Hatutaki kusikia mtanzania
amekosa fursa hii kwa sababu ya kukosa fedha …ukibahatika njoo kwenye
Baraza tutakushauri… Serikali ina mifuko 17 yenye fedha za kutosha
kukuwezesha” anaeleza Mkurugnezi wa uwezeshaji wa NEEC Bwana Edwin
Chrisant.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bwana Godfrey Simbeye
aliwaambia waandishi wa habari kuwa taasisi yake imejipanga kuhakikisha
kuwa mikataba ya kandarasi itakayofikiwa inazingatia maslahi ya pande
zote na utekelezaji wake unafanyika kulingana na vipengele vya mikataba.
Dhamira hizi zilizoelezwa na
taasisi hizi muhimu nchini, hapana shaka yoyote kuwa ni habari njema
inayoashiria matumaini makubwa na kuonesha sasa watanzania wameamka na
wamedhamiria kujenga Tanzania mpya kwa kila mmoja kwa nafasi yake
kuyatumia mazingira yaliyopo kujenga uchumi wa taifa.
Kama kweli taasisi hizi
zitatekeleza yale ziliyojipangia ikiwemo kuwapatia watoa huduma msaada
wa kitaalamu, huduma za kisheria, kifedha, viwango na vigezo katika
manunuzi, utaalamu, kuwaunganisha na wabia, kuwajengea uwezo vijana
wasomi ili waweze kushika nafasi zitakuwa zimetoa msaada mkubwa kwa
nchi.
Kwa hakika mradi huu kama
ilivyoelezwa awali utakuwa kigezo muhimu kupima utayari, umakini na
uwezo wa sekta binafsi kuchangamkia fursa zinapotokea na mafanikio ya
ushiriki wa sekta hiyo huenda ukawa mwanzo mzuri wa kuupa mgongo
utamaduni ulizoeleka wa watanzania kulalamika hususan kuilalamikia
Serikali kuwa haiwapi fursa kama hizi.
Wahenga walisema “shike shike na
mwenyewe nyuma” kwa hili Serikali zimefanya wajibu wake sasa mpira uko
kwa wadau katika sekta binafsi kuucheza kwa zitumia fursa na ni vyema
kukumbuka kuwa “mso matendo hula uvundo” hivyo watanzania wachangamkie
fursa wasije wakajikuta karamu imekwisha ‘wakaramba vyungu.
Ni vyema pia kutanabahisha kuwa
fursa za mradi huu haziko kwa watoa huduma kama hao pekee ambao wao ni
wafanyabiashara na wataalamu ambao tayari wanajielewa, wana uwezo na
wako katika sekta hiyo hivyo tunaweza kusema wana angalau uzoefu.
Lakini ukweli hi kuwa fursa za
mradi huu zimetapakaa kila mahala katika ngazi mbali mbali kuanzia
wakulima wa jembe la mkono, wafugaji wadogo wadogo, mafundi mchundo,
hadi vibarua wa ujenzi. Hivyo taasisi zinazohusika zinapaswa pia
kuliangalia kundi hili kubwa na kuhakikisha linashiriki vyema.
Hii ni kwa sababu, inapozungumziwa
ajira elfu kumi na ajira nyingine zaidi ya elfu thelathini nyingi
zinawagusa watanzania wa kundi hili. Ikumbukwe kuwa kundi hili ambalo
ndilo litakalokuwa karibu na mradi ndilo litakalokuwa la kwanza
kulalamika pindi litakapokosa fursa na kujikuta halina namna ya
kushiriki na kufaidika.
Utekelezaji mzuri na wenye ufanisi
wa mradi huu kwa kushirikisha sekta binafsi nchini utakuwa kigezo cha
kufungua milango kwa miradi mingine mikubwa ya aina hii humu nchini.
Watanzania hawana budi kumpongeza
Rais Magufuli kwa jitihada zake za kujenga Tanzania Mpya yenye matumaini
mapya. Hakika Tanzania yenye uchumi wa kati na ya viwanda inawezekana,
kama kila mmoja atatimiza wajibu wake.
No comments :
Post a Comment