Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla ameziagiza halmashauri
zote kuwafikisha mahakani na kuuza mali zao wadaiwa sugu wa kodi ya
pango la ardhi wenye madeni ya muda mrefu.
Dkt. Mabulla ametoa agizo hilo
wakati alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya makusanyo ya kodi ya ardhi
mkoani Geita mara baada ya kukuta majina 100 ya wadaiwa wa kodi ya ardhi
ambao hawajalipa kwa zaidi ya miaka 10.
Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi
alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kuhakikisha wadaiwa
hao wa muda mrefu wanaandikiwa notisi ya muda wa siku 14 na wasipolipa
ndani ya muda huo wafikishwe mahakamani bila kuchelewa na kama
wasipolipa basi mali zao zipigwe mnada.
Mara baada ya kubaini hayo Mhe.
Mabulla amefanya upekuzi wa nyaraka za umiliki wa ardhi katika masijala
ya ardhi ya Halmashauri ya mji wa Geita na kugundua uhifadhi mbovu wa
hati na ucheleweshwaji utoaji hati za wamiliki kwa muda mrefu.
Naibu waziri alimuagiza Mkurugenzi
wa Halmashauri ya mji wa Geita kutembelea mara kwa mara katika ofisi na
masijala za ardhi ili kuhakikisha maafisa wa idara ya ardhi wanatoa
hati kwa wakati na kwa mpangilio mzuri bila kuleta migogoro.
Aidha, Naibu Waziri huyo
alitembelea eneo lenye viwanja vilivyowekwa mpango wa matumizi bora ya
ardhi katika wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita ambavyo vimepangwa
kujengwa ofisi za serikali, shule, hospitali, makazi, maeneo ya kuzikia,
na huduma nyingine za kijamii.
Naibu Waziri alimtaka mkuu wa
wilaya ya Nyang’hwale kihakikisha mji huo unapangwa vizuri na kuwekwa
miundombinu ya barabara, maji safi na taka na umeme ili kuepusha
migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi huibuka kutokana na wilaya kutokuwa
na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya muda mrefu.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla
ametembelea eneo la Bombambili mkoani Geita lililojengwa nyumba 48 za
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo nyumba 14 tayari zimenunuliwa na
Halmashauri ya mji wa Geita.
Mhe. Mabulla alizitaka halmashauri
nyingine nchini kuiga mfano wa halmashauri ya mji wa Geita kwa
kuwashirikisha NHC katika kujenga nyumba bora badala ya kutumia
wakandarasi wa nje wakati Shirika la Nyumba la Taifa lipo na linajenga
nzuri na kwa gharama nafuu.
Naye Meneja wa NHC Mikoa ya
Mwanza, Geita na Simiyu Eng. Benedict Kilimba alimeishukuru Halmashauri
ya mji wa Geita kwa kuwa wakwanza kununua nyumba hizo 14 katika hatua ya
awali.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla anaendelea na ziara yake ya
mikoa ya kanda ya ziwa ambapo anataria kufanya ziara Mkoa wa Shinyanga
hasa katika wilaya ya Kahama na Shinyanga Mjini.
No comments :
Post a Comment