Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani (Kulia) akimweleza jambo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye
Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) alipotembelea Ofisi za Tume ya
Taifa ya Uchaguzi eneo la kuhifadhia Mashine za BVR. Katikati ni Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
akitazama moja ya Daftari la Wapiga Kura alipotembelea Ofisi za Tume ya
Taifa ya Uchaguzi jijini Dar es salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa
Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani na Kushoto ni Afisa TEHAMA wa Tume Bi.
Mwamvita Solo.
Afisa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Bw. Julius Kobelsiki akitoa ufafanuzi kuhusu Mashine ya
kuandikisha Wapiga Kura ya BVR kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
alipotembelea Ofisi za Tume jijini Dar es salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
akizungumza na baadhi ya watendaji na watumishi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Ofisi za Tume
jijini Dar es salaam. Kulia kwake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw.
Kailima Ramadhani (kulia).
Picha/ Aron Msigwa.
……………………………………
Na. Aron Msigwa
4/8/2017 Dar es slaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendelea kusimamia
matumizi bora ya rasilimali inazopewa na Serikali na kuzitaka taasisi
nyingine za Serikali kuiga mfano huo.
Mhe. Muhagama ameyasema hayo leo
jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Bunge kupitia Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Bora iliyoridhia Bunge
lipitishe fedha kiasi cha shilingi bilioni 10 kuiwezesha Tume kufanya
maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini .
Akizungumza na watendaji na baadhi
ya watumishi wa Tume amesema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wao na
namna Tume ilivyojipanga kutekeleza jukumu la uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura kuelekea uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa kuwa na
mpango Kazi, unaochambua na kubainisha mahitaji muhimu yanayotakiwa,
lini na wapi ili kazi hiyo iweze kufanyika kwa umakini.
“ Naipongeza sana Tume kwa
kuendelea kufanya vizuri , nimegundua kuwa imejipanga vizuri kutekeleza
majukumu yake ambayo yameainishwa Katika Katiba, kwa niaba ya Waziri
Mkuu nimekuja hapa na timu ya watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala Bora walioridhia Bunge lipitishe fedha shilingi Bilioni 10 ili
kuiwezesha kufanya maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura” Amesema.
Mhe. Mhagama ameeleza kuwa kazi
hiyo kazi ya utekelezaji wa maagizo hayo ya Bunge inazingatia Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 5 kifungu kidogo
cha 3 (a) ambacho kimeweka uanzishwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura nchini na Ibara ya 74 kifungu kidogo cha 6 (a) na (e) ambacho
kinaipa Tume madaraka ya kuchukua jukumu la kuandikisha wapiga Kura
nchini Tanzania.
Aidha, ameongeza kuwa Sheria ya
Uchaguzi kifungu cha 15 (3) kinaipa madaraka Tume ya Uchaguzi
kutengeneza mfumo na utaratibu wa uandikishaji wa wapiga Kura nchini na
uboreshaji wa daftari hilo mara mbili kati ya Uchaguzi mkuu mmoja na
unaofuata.
“Tunaelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2020 kwa hiyo ili tuzingatie takwa la Katiba na takwa la Sheria ya
Uchaguzi ambayo inasimamiwa na Tume ni lazima sasa Serikali ione kwamba
inaisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wote tunajua kuwa utendaji wake
ni huru lakini Serikali tunaowajibu wa kuhakikisha kuwa Tume inafanya
kazi yake vizuri” Amesisitiza.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi akizungumza mara
baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ameipongeza uongozi wa Tume kwa
kuonyesha mfano katika kuondoa mazoea katika utendaji kazi ikiwemo
utunzaji wa mali na rasilimali za Serikali.
Amesema kuwa Serikali itaendelea
kuijengea uwezo Tume kwa kuipatia rasilimali na vitendea kazi
inavyohitaji ili iweze kutimiza majukumu yake kwa wakati.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akizungumza mara baada
ya kumalizika kwa ziara hiyo amemshukuru viongozi hao kwa kuzitembelea
ofisi za Tume kuangalia maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura na kuishukuru Serikali kwa kutenga shilingi Bilioni 10
zitakazotumika kwa ajili ya uboreshaji huo.
Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi imejipanga kulitekeleza jukumu hilo kikamilifu na inaendelea
kufanya maandalizi mbalimbali yakiwemo ya kuzipitia Mashine za BVR
zitakazotumika kuandikisha wapiga Kura , kupitia mifumo Sheria na kanuni
za Uboreshaji, kupitia vifaa vilivyopo ili kupunguza mzigo wa kununua
vifaa vipya wakati wa zoezi hilo.
No comments :
Post a Comment