BENNY
MWAIPAJA, WFM, MTWARA
BENKI
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeelezea kuridhishwa na kasi pamoja na viwango
vya miradi ya ujenzi ya barabara inayofadhiliwa na benki hiyo katika Ukanda wa
Kusini, na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili
kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na wananchi wake.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo anayesimamia Kanda wa Afrika
Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, (pichani anayezungumza), baada ya kutembelea na kukagua barabara ya
Tunduru-Nangaka-Mtambaswala, mkoani Mtwara, yenye urefu wa kilometa 202.2.
Barabara
hiyo yenye vipande vitatu imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 180 kupitia
ufadhili wa benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA)
na Serikali ya Tanzania.
Dkt.
Weggoro amesema kuwa barabara hiyo ambayo upande mmoja inaunganisha Tanzania na
Msumbiji, itachochea maendeleo ya wananchi kutoka pande hizo mbili kwa
kusafirisha watu na bidhaa kwa urahisi zaidi.
“Nimeona
mabadiliko makubwa sana, si tu kwa barabara, lakini maisha ya watu, mabadiliko
ambayo ni dhahiri yanatokana na hii miradi ya barabara ambayo imefungua fursa
nyingi za maendeleo, watu wanafanyabiashara lakini pia wanatembeleana!” alisema
Dkt. Weggoro.
Alitoa
wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa barabara hizo kujiletea
maendeleo kwa kufanyabiashara hivyo kujikwamua kiuchumi.
Mhandisi
Heldaus Jerome kutoka Wakala wa Barabara -Tanroads, Makao Makuu, alisema kuwa
barabara hiyo ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala, ina vipande vitatu, kutoka
Mangaka – Nakapanya (km 70.5), Nakapanya – Tunduru (66.5) na Mangaka –
Mtambaswala (km 65.5)
Alifafanua
kuwa gharama za ujenzi wa mradi huo, kiasi cha Dola milioni 210, kimetolewa na
AfDB (64.79%), Shirika la Maendeleo la Japan-JICA (32.83%) na Serikali ya
Tanzania (2.38%) na kwamba Wadau hao pia wanafadhili ujenzi wa barabara kutoka
Dodoma-Babati yenye urefu wa kilometa 180.53.
Baadhi
ya wakazi wa mji wa Mangaka wilayani Masasi mkoani Mtwara, wameishukuru
Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa uchumi na maisha
yao kwa ujumla kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo
ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Kilimanihewa, Bw. Abbas Muhidin Mwira, alisema kuwa maeneo ya
Mangaka yamechangamka kibiashara na vijana wengi wamejiajiri wenyewe kwa kufanyabiashara
zinazowaingizia kipato huku huduma za usafiri zikiboreshwa baada ya mabasi ya
abiria yaendayo mikoani pamoja na malori yanayobeba saruji kutoka Kiwanda cha
Saruji cha Dangote-Mtwara kuanza kupita njia hiyo na kusisimua biashara zao.
No comments :
Post a Comment