Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga (aliyesimama) akifungua Warsha ya Siku Mbili ya
Wadau wa Vyama vya Ushirika inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Benki
Kuu Tawi la Mtwara, Bw. Lucas Mwimo (kushoto) na Kaimu Katibu Tawala
Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji, Bw. Amani Rusake (kulia).
Mkurugenzi wa Biashara wa Mikopo
wa TADB, Bw. Augustino Chacha akiwasilisha mada kuhusu mchango wa TADB
katika mapinduzi ya kilimo nchini.
Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya
Ushirika Nchini, Bw. Nerei Kyara akizungumza na Wadau wa Vyama vya
Ushirika wakati wa Warsha ya Siku Mbili ya Wadau inayoendelea katika
Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Wengine pichani
ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji, Bw. Amani Rusake
(kushoto) na Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa Mfuko wa Kukuza Sekta
ya Fedha, Bw. Mwombeki Baregu.
Wadau wa Vyama vya Ushirika
wakifuatilia mijadala mbalimbali wakati wa Warsha ya Siku Mbili ya Wadau
inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara.
Wadau wa Vyama vya Ushirika wakiwa
katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa Warsha ya Siku Mbili
ya Wadau hao inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara.
………………………..
Na Mwandishi wetu, Mtwara
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imewaasa wakulima wa korosho nchini kuongeza uzalishaji
wa korosho ili kuchangamkia fursa za masoko ya zao hilo linalohitajika...
zaidi katika masoko ya Marekani, Vietnam na India.
Wito huo umetolewa jana na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akifungua Warsha
ya Siku Mbili ya Wadau wa Vyama vya Ushirika inayoendelea katika Ukumbi
wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Bw. Assenga alisema kuwa mahitaji
ya korosho ni makubwa sana katika soko la dunia hivyo wakulima wa zao
hilo hawana budi kujizatiti ili kuhakikisha wanazalisha kiasi kikubwa
cha korosho ili kufikia au kuzidi malengo ya mavuno kwa msimu ujao
ambayo yanakadiriwa kufikia kati ya tani laki tatu (3) hadi laki nne (4)
ukilinganisha na takribani tani laki mbili na nusu kwa msimu uliopita.
Bw. Assenga alisema kuwa korosho
ni zao la kimkakati ambalo likiwekezwa kwa usahihi linaweza kunyanyua
uchumi na kipato kwa wakulima wa mikoa ya kusini na pwani ambao niyo ni
wazalishaji wakuu wa zao hilo.
“Nawaasa mujitahidi kulima kisasa
ili kuweza kufikia au kuvuka malengo ya mavuno ya msimu huu hali
itakayowaongezea kipato hivyo kufikia malengo ya serikali ya kuwanyanyua
wakulima nchini,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa TADB
aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kusaidia mfumo wa Stakabadhi ya
maghala ili kuhakikisha kuwa malengo ya mavuno ya korosho kwa msimu huu
yanafikiwa.
“TADB iko tayari kuratibu mfumo wa
malipo ya fedha zitokanazo na mauzo ya korosho kwa njia ya TEHAMA, pia
kwa kushiriakiana na soko la mazao (TMX), kusimamia ununuzi wa mazao kwa
njia ya mtandao (electronic auction),” aliongeza
Aliongeza kuwa Benki ipo tayari
kusimamia uuzaji wa mazao kwa mifumo ya salama ya kimataifa ya malipo
kama vile dhamana ya malipo.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa
Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema kuwa Benki ya Kilimo ipo
tayari kutoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya
umwagiliaji na maghala na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho
na mihogo.
Aliongeza kuwa TADB pia ipo tayari
kuviwezesha viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta,
mihogo pamoja na uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya korosho
na ufuta.
“Tupo tayari kutoa mikopo kwa
ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali kupitia
mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya
umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo (kama matrekta, pump),”
alisema.
Bw. Chacha aliongeza kuwa kwa
kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazao ya kilimo, Benki ya Kilimo ipo
tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kujenga maghala mapya au kuboresha
yaliyopo pamoja na kununua mizani ya kisasa na ununuzi wa magari ya
usafirishaji mazao.
No comments :
Post a Comment