Na Mwandishi wetu Songwe
Taasisi ya Kimataifa ya kijamii ya
uhifadhi wa wanyamapori ya World Concervation Society- WCS imetoa
msaada wa zaidi ya shilingi milioni 936 kwa mapori ya akiba ya Lukwati-
Piti ambazo zimetumika kujenga jengo la kisasa la ofisi, ununuzi wa
magari matatu ya doria na kuendesha mafunzo ya askari wa wanyamapori wa
mapori hayo yaliyoko mkoani Songwe.
Akiongea katika halfa ya kukabidhi
miradi hiyo kwa serikali ya Tanzania, Mkurugenzi wa
WCS Aaron Nicholaus
amesema taaisisi hiyo inajivunia kushirikiana na serikali ya Tanzania
katika kuendeleza shughuli za uhifadhi wa wanayamapori wakiwemo tembo
ambao ni maliasili muhimu kitaifa na kimataifa ambapo shirika la misaada
la watu wa Marekani USAID nalo ni mdau mkubwa katika ufadhili huo.
Bwana Nicholaus alisema msaada huo
umetilia mkazo suala la mafuzo ambayo yatawaongezea askari ujuzi na
weledi wa kukabiliana na majangili ambao wamekuwa wakiua tembo na
wanyamapori wengine kwa maslahi yao binafsi na kusababisha hasara kwa
serikali ambayo inawategemea wanyamapori kwa maendeleo ya jamii na
taifa.
“Tunapofikiria uhifadhi, tuangalie
pia masuala ya mapito ya wanyamapori kama tembo ambayo yamekuwa
yakitoweka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu na hivyo
kuathiri uhifadhi maana tembo huhitaji eneo kubwa kwa malisho” alisme
abwana Nicholaus.
Taarifa ya miradi hiyo iliyotolewa
kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudance
Milanzi ilieleza kuwa miradi hiyo ina thamani kubwa kwa uhifadhi wa
mapori hayo yenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 6,119 ambayo
yanapakana na Hifadhi ya taifa ya Ruaha na pori la akiba la Rungwa
Meneja wa Mapori ya Lukwati Piti
Bwana Alphonce Ambroce Mung’ong’o akitoa ufafanuzo na mchanganuo wa
gharama za miradi hiyo alisema jengo la kisasa la ofisi limegharimu
zaidi ya shilingi milioni 227, magari matatu kwaajili ya doria yana
thamni ya dola 255,000 za kimarekani boti na mfumo wa radio call una
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 234.
Aidha Bwana Ambroce alisema
wafadhili hao pia wamenunua boti mbili za doria ambazo zimegharimu zaidi
ya shilingi milioni 134 ambazo zitatumika kuimarisha doria katika ziwa
Rukwa ambalo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya mapori hayo ya Lukwati
Piti.
Kuhusu ujangili, Bwana Ambroce
alisema katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2013 mpaka sasa
zaidi ya tembo 23 wameuwawa kwa ujangili katika mapori hayo ingawa
alisema kwa sasa baada ya mafunzo hayo mapori hayo yameimarisha doria na
amewaonya majangili kuwa sasa serikali imejipanga kupambana nao
kikamilifu.
“Nawaonya majangili, sasa
tumejipanga kupambana nao na kamwe hatuwezi kuwaacha waendelee kutamba
humu na kumaliza rasilimali zetu kwa manufaa yao, hii haikubaliki na
kamwe hatutawavumilia, tumepata mafunzo na vitendea kazi lazima
tutashinda na kuwaacha wanyamapori watumike kwa shughuli za kitaifa na
kwa maslahi ya watanzania walio wengi” alisisitiza Ambroce.
Akiongea baada ya kupokea misaada
hiyo, Katibu Mkuu wizara ya maliasili na utalii Meja Jenerali Gaudance
Milazi amewashukuru wadau wa uhifadhi ikiwemo WCS kwa kusaidia juhudi za
kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania kwani mchango wao
umeanza kuzaa matunda.
Meja Jenerali Gaudance Milanzi
alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za wanyamapori wengi sana
ambao wakitunzwa na kutumika vizuri wana nafasi kubwa ya kuchangia kwa
kiwango kikubwa kuliondoa taifa katika umasikini uliokithiri na hivyo
kuchangia kwa kiwango kikubwa kaika pato la taifa na maendeleo ya nchi.
“Kazi kubwa tuliyonayo ni
kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa ipasavyo kwa manufaa ya vizazi
vyote na kamwe asiwepo mtu mwenye uroho wa kutumia rasilimali hizi kwa
manufaa yake binafsi” alisisitiza Meja Jenrali Gaudance Milanzi.
Alisema anatambua kabla ya kituo
cha Lukwati Piti kuanza mwaka 2013 wavuvi walikuwa wamesheheni katika
fukwe za ziwa Rukwa upande wa pori la akiba la Likwati, “Hivi sasa kambi
hizo za wavuvi zilishaondolewa na fukwe hizo zimebaki kuwa mazalia
mazuri ya mamba ya samaki na malisho ya wanyamapori hali inayoleta
matumaini ya kuimarika kwa uhifadhi wa wanyamapori” alisema Meja
jenerali Milanzi.
Meja jenerali Gudance Milanzi
alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wananchi wakorofi wajiepushe
kufanya za binadamu ikiwemo uanzishaji wa makazi, kilimo, uvuvi,
uchimbaji wa madini na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa
kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za uhifadhi.
“Sasa maeneo mengi ya hifadhi
yanakumbwa na changamoto za ongezeko la shughuli za binadamu ikiwemo
uingizaji wa mifug itambulike kwamba maeneo ya hifadi yametengwa
kisheria kwa shughuli za uhifadhi na wanaofanya mchezo huo waache mara
moja na sheria itaendelea kuchukua mkono wake kwa wafugaji na mifugo
inayokamatwa” alionya.
Meja jenerali Gudance Milanzi
alisema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha
masuala ya ujangili yanadhibitiwa ikiwa ni kuweka mazingira mazuri ya
utendaji kazi kwa watumishi wake, kununua vitendea kazi ikiwemo magari
ya doria.
Alisema juhudi hizo ni pamoja na
kugeuza mfumo wa kiutendaji kutoka ule kiraia na kwenda mfumo wa jeshi
usu na akaipongeza Mamlaka ya wanyamapori TAWA kwa kutoa kipaumbele
katika mafunzo kuelekea mfumo wa jeshi usu ambapo katika kipindi cha
mwaka mmoja TAWA imetoa mafunzo kwa watumishi 236.
Mapema katika taarifa yake kwenye
hafla ya kupokea miradi hiyo kutoka WCS iliyofanyika kwenye ofisi za
pori hilo zilizoko Lupatingatinga wilayani Songwe, kaimu Mkurugenzi mkuu
wa mamlaka ya Wanyamapori TAWA Martini Loibooki alisema ufadhi wa WCS
katika mapori hayo ni matokeo ya ushirikiano unaoendelea kati ya TAWA na
wadau wa uhifadhi.
Bwana Loibooki alisema WCS imekuwa
mfadhili wa kwanza kuingia kufadhili mapori ya Lukwati Piti ambayo hko
nyuma yalikuwa na changamoto nyingi ikiwemo ujangili na uwindaji haramu
lakini kutokana na ufadhili huo sasa uhifadhi umeanza kuimarika.
Alisema amepokea changamoto za
kituo cha Lukwati Piti lakini Mamlaka imeweka mipango ya muda mfupi na
muda mrefu kuhakikisha changamoto hizo zinaendelea kupungua kadri
upatikanaji wa fedha na kwamba mazingira ya kazi yameanza kuwa bora na
vitendea kazi vimeongezeka na kuwa bora kuliko miaka ya nyuma.
Alieleza kuwa mapori ya Lukwati
Piti yana umuhimu mkubwa na yamekuwa chanco muhimu cha mapato ya
serikali kutokana na uwindaji wa kitalii ambapo katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita mapori hayo yameliingizia taifa mapato ya zaidi ya
shilingi bilioni mbili na milioni mia tisa.
Bwana Loibooki alisema fedha hizo
zinazotokana na uwindaji wa kitalii ni nyingi na zimeisaidia serikali
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mikoa mbalimbali nchini
ikiwemo afya , elimu na ujenzi wa miradi ya kijamii.
No comments :
Post a Comment