*Heroine, Cocaine, bangi, mirungi na kemikali bashirifu vyakamatwa
* Mashamba ya bangi ekari 569.25 na mirungi ekari 64.5 yateketezwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema katika kipindi cha miezi minne, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini (DCEA) imewakamata watuhumiwa 4,809 na
kufungua majalada
ya kesi 3,222.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja
ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi
Septemba 5, mwaka huu.
“Katika kipindi kifupi tangu
Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata
watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu
327.173); cocaine (kilo 26.977); bangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo
11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini,”
amesema.
Amesema mamlaka hiyo kwa
kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za
kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bangi na ekari 64.5 za mashamba
ya mirungi na kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya
majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.
“Dawa za kulevya zina athari
kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda
kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali
katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wote
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Amesema azma ya Serikali ya
awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini kwa
kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa endelevu,
yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. “Tuungeni mkono kwenye
mapambano haya, ili tutokomeze kabisa mtandao huo,” amesisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 – DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017.
No comments :
Post a Comment