Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiongea na wananchi
waliojitokeza kulipa kodi ya majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA)-Ilala Mtaa wa Kipata, na kuwapongeza kwa kuitikia wito
huo kwa wingi na kuwaeleza kuwa kwa kulipa kodi kutasaidia upatikanaji
wa huduma muhimu kama maji, barabara, umeme na dawa hospitalini.
Wananchi waliofika katika Ofisi
za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata, wakimsikiliza
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia)
akiwaelezea namna atakavyoboresha huduma kwa walipa kodi za majengo kwa
kuwapa kipaumbele walemavu, wazee, wagonjwa na wasiojiweza. Tukio hili
litaenda sambamba na kuwawekea sehemu maalumu ya kukaa wakati wakisubiri
huduma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akipokea shukrani na pongezi
kutoka kwa Bi. Rose Muyalo, kwa utendaji makini wa Serikali ya Awamu ya
Tano na kwa kupatiwa huduma bora kutoka kwa wafanyakazi wa TRA.
Bw. Obedi Hezron Misoji (kulia)
ambaye ni mstaafu akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) (kushoto), kuongeza muda wa zoezi hili la ulipaji kodi
ya majengo kwani watu bado ni wengi na Watanzania wameonesha nia
yakujitokeza kwa wingi kulipia kodi hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia) akiongea na wananchi waliofika
katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata
kulipa kodi za majengo na kuelezea furaha yake namna walivyoitikia wito
huo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akiwasikiliza viongozi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata namna ambavyo
wanaweza kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo katika zoezi
hili la ulipaji kodi wa Majengo. Kutoka kulia ni Meneja Msaidizi Kanda
ya Ilala kwa upande wa madeni Bw. Nuhu Ramadhani, Meneja wa Kanda ya
Ilala Bw. Abdul Mapembe na Bw. Revelian Kajuna.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akisalimiana na mmoja wa
wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)- Mbagala, alipotembelea
ofisi hizo kujionea namna zoezi la ulipaji kodi ya majengo unavyoendele
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwa katika moja ya ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA)- Mbagala na kukutana na Mtoto Salma (aliyembeba)
ambaye aliambatana na mama yake (hayuko pichani) kwenda ofisini hapo
kulipa kodi ya majengo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akiongea na baadhi ya wazee
waliojitokeza kulipa kodi za majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA)- Mbagala jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akiwapongeza vijana
waliojitokeza kulipa kodi ya majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) – Mbagala jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
………………………………………………………………………
Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam
Zikiwa zimebaki siku tatu kati ya
siku 15 zilizoongezwa na Serikali kwa wananchi kulipa kodi ya majengo
bila adhabu, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameiomba
Serikali iongeze muda mwingine zaidi ili watu wote waweze kulipa kodi
hiyo bila adhabu kutokana na
changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati
wa zoezi hilo.
Wananchi hao wamemweleza Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipofanya ziara za kushitukiza
katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA-Mtaa wa Kipata-eneo la
Mnazi Mmoja na Mbagala mkoani Dar es Salaam
Wamesema kuwa mwamko wa wananchi
kulipa kodi ni mkubwa hali iliyosababisha foleni kubwa kila mahali
nchini kutokana na uhaba wa watumishi wa TRA pamoja na vitendeakazi
muhimu kama vile kompyuta na mashine za kielektroniki za kutolea risiti
(EFDs).
Waziri wa Fedha na Mipango Dokta
Philip Mpango amewataka Watanzania kuwa watulivu na kuendelea kulipa
kodi hiyo huku akiahidi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja
na vitendeakazi ili kuwaondolea adha wananchi waliojitokeza kwa moyo
kulipa kodi mbalimbali ikiwemo ya majengo.
Ameahidi pia kwamba Serikali
itayafanyiakazi maombi ya wananchi ya kutaka kuongezewa muda wa kulipa
kodi hiyo na kwamba watajulishwa wakati muafaka uamuzi wa Serikali
kuhusu suala hilo.
Dokta Philip Mpango amesema kuwa
Serikali inafarijika kwa kiasi kikubwa na namna wananchi walivyoitikia
wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli unao wataka
wananchi walipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Amebainisha kuwa watu wanapolipa
kodi wanaipa nguvu Serikali ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi
ikiwemo elimu, barabara, maji, afya na kuboresha huduma ya umeme hususan
vijijini na kulifanya Taifa kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje
ya nchi.
Majuma mawili yaliyopita Serikali
iliongeza muda kwa wananchi kulipa kodi ya majengo bila adhabu kwa muda
wa majuma mawili hadi Julai 15 mwaka huu ambapo siku hizo zitaisha siku
ya Jumamosi huku idadi kubwa ya watu ikiwa bado wanahitaji kulipa kodi
hiyo.
No comments :
Post a Comment