NA IS-HAKA OMAR-ZANZIBAR.
JUMLA ya Pikipiki 14 aina ya Vespa
zenye thamani ya shilingi milioni 37 zimetolewa na Mbuge wa jimbo la
Kiwengwa Khamis Mtumwa kwa Makatibu wa Matawi ya CCM ya jimbo hilo.
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhi vitendea kazi hivyo huko katika uwanja wa mpira wa
kwa Gube,
mbunge huyo alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi wa
jimbo hilo.
Alieleza kwamba lengo la kutoa
vifaa hivyo ni kuwarahisishia huduma za usafiri watendaji hao ambao
muda mwingi wanakuwa na majukumu mbali mbali yanayohitaji usafiri wa
haraka ili yaweze kutekelezwa kwa wakati.
Aliahidi kuwa hiyo ni sehemu tu ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jimbo hivyo ataendelea kutatua
kero mbali mbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
“ Nitaendelea kumarisha huduma
mbali mbali za kijamiii kadri mwenyezi mungu atakavyonijaalia, wito
wangu kwenu ni kwamba miradi ambayo kwa sasa naitekeleza katika jimbo
hili mnatakiwa kuitunza ili iweze kuwanufaisha watu wote.”, alisisitiza
Khamis.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ mara baada ya
kukabidhi Pikipiki hizo kwa watendaji hao aliwataka viongozi wa
majimbo ya chama hicho kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbali
mbali ya maendeleo kwa wananchi.
Alisema kwa sasa viongozi
wanatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015/2020 kwa vitendo ili wananchi waone maendeleo yanayofanywa
na viongozi wao.
Alisisitiza kuwa ni lazima
viongozi wa majimbo waende na wakati Kwa kutangaza na kutoa taarifa za
uhakika juu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM , hatua itakayosaidia kujenga
imani za wananchi waliowachagua katika uchaguzi mkuu uliopita.
“ Naendelea kuwakumbusha baadhi ya
wabunge, wawakilishi na madiwani ambao bado utekelezaji wao wa Ilani ya
Chama chetu unasuasua katika majimbo yao kuwa waanze kurudi kwa
wananchi kutekeleza yale waliyowaahidi kabla ya uchaguzi mkuu ujao”,
alisema Dkt. Mabodi.
Nao baadhi ya makatibu mbali mbali
waliokabidhiwa vifaa hivyo wameahidi kuvitumia vizuri kwa lengo la
kuimarisha shughuli mbali mbali za chama hicho.
No comments :
Post a Comment