WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali haitamsamehe mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhilifu
wa mali za fedha za Ushirika nchini.
“Kwa Serikali hii ya awamu ya Tano
tutachua hatua kali kwa wezi wa mali na fedha za
ushirika na
tunaendelea kufanya usafi wa wabadhilifu hadi tupate viongozi
waadilifu,”.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumamosi, Julai Mosi, 2017), katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika
Duniani (SUD), iliyoadhimishwa kitaifa mjini Dodoma kwenye ukumbi wa
Jakaya Kikwete.
Amesema miongoni mwa changamoto
zinazoukabili Ushirika nchini ni pamoja na wizi na ubadhilifu wa
rasilimali za Ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama
wasiokuwa waaminifu.
Waziri Mkuu amesema changamoto
nyingine ni baadhi ya viongozi wa vyama vya Ushirika kutoheshimu
miongozo ya vyama vyao na kujifanyia mambo kwa maslahi yao binafsi.
Amesema katika kukabiliana na
changamoto hizo Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake na kuweka
mazingira rafiki ya kustawisha Ushirika nchini ili kutoa fursa ya
Ushirika kushamiri na kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi
yao.
“Haikubaliki hata kidogo kuona
sekta hii inayosadifu maisha ya Mwafrika hamnufaishi ipasavyo , hivyo
naelekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini ihakikishe kuwa vyama vya
Ushirika vinaendeshwa kisayansi na kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Pia amezielekeza Kamati za Ushauri
za Mikoa na Wilaya nchini, ziingize agenda ya Maendeleo ya Ushirika
kama moja ya agenda muhimu inayopaswa kujadiliwa na kuwekewa maazimio ya
utekelezaji. Pia wawe na takwimu za vyama vya Ushirika na Wanaushirika.
Hata hivyo Waziri Mkuu
amezielekeza mamlaka zote zinazohusika na Ushirika nchini zijiwekee
malengo yanayopimika ya namna ya kuboresha sekta ya Ushirika.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameelekeza kwamba masuala yote yanayohusu Ushirika wa kilimo nchini
lazima yaratibiwe na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aidha, Waziri Mkuu amezielekeza
Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zifanye
mapitio kubaini elimu na ujuzi katika ngazi zote za Ushirika kwa ajili
ya kuwaandalia kozi za muda mfupi za kuongeza ujuzi au kubainisha aina
ya watumishi wanaohitajika kwenye sekta hiyo.
Pia amewaagiza Maofisa Ushirika
nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri uchanguzi wa Vyama vya Ushirika
vya Msingi (AMCOS) na kuwaondoa wagombea wote waliowahi kuwa viongozi,
ambao waliondolewa madarakani kutokana na ubadhilifu wa mali na fedha za
Ushirika.
Awali, Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alisema wizara itaendelea kusima na kuchukua
hatua kwa viongozi wote wa vyama vya Ushirika watakaobainika kufuja
mali na fedha za Ushirika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, JULAI 1, 2017
No comments :
Post a Comment