Thursday, June 29, 2017

WANACCM KIBITI,WAILILIA CCM TAIFA KUAHIRISHA UCHAGUZI WA NDANI


KIBINa Mwamvua Mwinyi ,Pwani
BAADHI ya wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM)wilayani Kibiti na Rufiji,mkoani Pwani ,wameutaka uongozi wa CCM Taifa kuangalia namna ya kuahirisha uchaguzi wa chama kwenye wilaya hizo ama mkoa kijumla .
Wameeleza hatua hiyo itawezesha wanachama kujipanga kwa wakati mwingine ili
kupisha kadhia ya mpito ya vitendo vya mauaji vinavyoendelea .
Aidha wamesema vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo na uchumi wilayani humo na kukwamisha mipango ya kikanuni na taratibu za vyama walizojipangia .
Hata hivyo ,wamesisitiza uwezekano wa vyama vya siasa vikubwa wilayani hapo, kukaa kwa pamoja na wazee wa pande zote kukemea vitendo hivyo.
Wakazi hao walibainisha kwamba,kwa umoja wao kutawezesha kushirikiana na serikali kumaliza janga hilo.
Muenezi wa Ccm wilaya ya Rufiji ,Musa Mnyelesa ,mkazi wa Kibiti Hadija Issa ,Hamis Kidongezo na Seif Mohammed waliyasema hayo,baada ya kutokea mauaji ya mwenyekiti wa kijiji na mtendaji Wa kijiji cha Mangwi ,Mchukwi usiku wa kuamkia June 28 .
Walieleza ,hadi sasa hakuna uchaguzi uliofanyika wa ngazi za chini ambako maeneo mengine unafanyika ,hakuna anaechukua fomu ya kugombea .
Wanaongeza kuwa kila mwanachama anahaki ya kugombea na kupiga kura ili kuimarisha chama chochote kile .
Walisema kutokana na vitendo vinavyotia shaka na kuonyesha Kibiti na Rufiji kutokuwa shwari ,ni vyema uchaguzi ukaahirishwa ili baadae kupata haki za kichama wakiwa na amani .
Muenezi wa CCM Rufiji ,alisema chama mkoa na taifa wanapaswa kutupia macho suala hilo kwa upana kwa maslahi ya chama .
Mnyelesa alisema serikali na askari polisi wanafanyakazi nzuri lakini inabidi kujulikane kina cha tatizo.
“Naona kuna haja ya vyama vyote vikaguswa na hili ,maana hii agenda lisingekuwepo bunge ina maana viongozi wa vya vingine vinavyokuwa na sauti kubwa ya kutetea mengi wasingeongeaa”
“Tunaomba wanasiasa ,viongozi wa dini ,wanaharakati washikane mkono kuongeza juhudi za kupiga kelele kwa hili kama ilivyo katika mambo mengine ya kijamii wanavyofanya” alisema Mnyelesa.
Mnyelesa alielezea kwamba ,bado wananchi ambao ni wanachama na viongozi wa CCM, vitongoji na vijiji wanaishi kwa hofu .
Nae Seif, alisema baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wanashindwa kwenda ofisini kutekeleza majukumu yao.
Alisema wanaishi kwa sintofahamu na imani inawatoweka.
Anaeleza miaka ya nyuma watu walikuwa wakigombea nafasi mbalimbali za uongozi lakini kwa sasa wanakwepa na kuhofia uhai wao,na anahofu hata uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 kuwa wengi hawatajitokeza.
Hadija aliiomba serikali kuwadhibiti wahamiaji haramu kwa kuwarudisha makwao badala ya kuachiwa kwani yawezekana wakaleta athari kubwa ndani ya Mkoa na taifa kijumla .
 Hadija alisema pia tatizo la wafugaji na wakulima liangaliwe kwani isije ikawa linachangia.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, aliwaomba wananchi washirikiane na serikali kuwafichua wahalifu .
Ndikilo ,alieleza wauaji ama wahalifu wapo ndani ya jamii hivyo endapo wananchi wataamua kuwataja watu hao itawasaidia kuwakamata kirahisi.
Mkuu huyo wa Mkoa ,aliwataka kuwasema pia wageni kwenye maeneo yao kwani wageni wengine sio watu wema.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga alibainisha kwamba,wanaendelea kupambana na kuimarisha ulinzi .
Ni matukio takriban 37  ya mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama, wenyeviti wa vijiji /vitongoji na askari polisi ambayo yanadaiwa kujitokeza wilayani Rufiji ,Mkuranga na Kibiti,tangu mwaka 2015.
Katika matukio hayo ni pamoja la March 28 ambapo mwenyekiti wa (CCM) tawi la  Mparange na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini ,Michael Lukanda,aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwani .
Jingine ni march 12,mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo Hemed Njiwa aliuawa kwa kupigwa risasi.
Jan 19,mjumbe wa serikali ya kijiji cha Nyambunda ,Oswald Mrope, aliuawa kwa kupigwa risasi.
March 1,mwenyekiti wa kijiji cha Nyambunda Said Mbwana aliuawa.
Feb 24,watu watatu akiwemo afisa upelelezi wa polisi wilaya ya Kibiti Peter Kubezya aliuawa kwa risasi.
April 13 mwaka huu,yalitokea mauaji ya askari polisi nane waliouawa kwa kupigwa risasi na wahalifu waliokuwa na silaha za moto .
Octoba 24,2016 afisa mtendaji wa kijiji cha Nyambunda Ally Milandu alipigwa risasi na kufa.
Novemba 6,2016 ,mwenyekiti wa kitongoji cha Nyang’unda kijiji cha Nyambunda Mohammed Thabiti alipigwa risasi akielekea kwake.
Matukio mengine ni sanjali na May 17 ,mwenyekiti wa CCM tawi la Njianne ,kijiji cha Muyuyu ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya siasa kata ya Mtunda ,Iddi Kilungi ,aliuawa kwa kupigwa risasi.
May 13 mwaka huu,katibu wa CCM kata ya Bungu ,wilayani humo,Halife Mtulia ,kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
June 28 mwaka 2017 ,mtendaji wa kijiji cha Mangwi,Shamte Makawa na mwenyekiti wa kijiji ,Hamis Mkima waliuawa na nyumba tatu kuchomwa moto.
Na june 21 mwaka huu,askari Polisi wawili wa kikosi cha usalama wa Barabarani wilayani Kibiti ,waligwa risasi na watu wasiojulikana katika kijiji cha Msafiri .

No comments :

Post a Comment