Friday, June 30, 2017

UVCCM WAWAWASHIA MOTO WAZEE WA CHADEMA

 Kaimu katibu Mkuu UVCCM Shaka Hamdu Shaka (wa katikati) akizungumza na waandishi wa Vyombo vya Habari  Ofisi ya UVCCM Upanga dar es Salaam
            waandishi na Viongozi Mbalambali wa UVCCM Wakisikiliza


TAARIFA ILIYOTOLEWA NA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA
MAPINDUZI (UVCCM) KWA VYOMBO VYA HABARI, IJUMAA30 JUNI 2017 UVCCM
UPANGA, DAR ES SALAAM
 

Ndugu Waandishi wa Habari

Kwa heshima kubwa tunawashukuru kwa dhati na kwa uungwana
wenu wa kuitikia wito wetu wa kuwaomba  kuhudhuria mkutano wetu huu  ili
kuzumgumza nanyi kama ilivyo ada na kawaida na hatimaye muweze
kufikisha ujumbe wetu kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

 
Ndugu Wandishi wa Habari

Itakumbukwa  kuwa hivi karibuni katika moja ya  Baraza la
Idd El Fitri lililofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijijini Dar
es Salam, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM,
Mzee Ali Hassan Mwinyi, alitoa maoni yake binafsi  baada ya kuutazama,
kuudurusu na kuridhika  na utendaji wa Serikali ya Awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli.
 

Ni ukweli usiofichika  wala kupingika kuwa  maoni ya Mzee
Mwinyi bila shaka yoyote yatakuwa yamepata mshawasha baada ya kuvutiwa
mno na uchapakazi wa Rais Magufuli, pia maoni hayo hayakuwa ni uamuzi
wala shuruti kama ambavyo baadhi ya watu walivyokishilia bango na
kulishupalia suala hilo kwa mtazamo hasi.

Maoni ya Mzee Mwinyi yalikuwa bayana au kwa lugha nyingine
ni maoni mubashara yanayoweza kumlazimisha kila binadamu mwenye akili
timamu afahamu kwa yakini alichotamka  katika matamshi yake. Alichosema
au kushauri ni  jambo lenye  mantiki kulingana na mtazamo wake  ambao
kwa hakika ulijiegemeza chini ya uhalisia wa mazingira ya nyakati na
utendaji wa Rais Dk John Pombe Joseph  Magufuli  kwa kadri
unavyoonekana.
 

Kwa bahati mbaya sana, eti wanaojiita ni wazee wa CHADEMA
bila kufanya tafakuri, uchambuzi wa maana katika dhana kamili yenye
uyakinifu wa jambo hilo, jana wakajikuta wakikurupuka, na kumuandama
Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi bila ya kuwa na sababu za msingi kwa
kumtolea maneno yasiyo na kichwa wala miguu. 

Tokea Rais Dk  John Pombe Magufuli aingie madarakani
baada  kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi mwaka 2015, sasa yapata
miaka miwili, utendaji wa Serikali yake ya awamu ya tano licha ya
kumvutia kila mtanzania, umeitikisa na kuamsha mjadala nchini, Afrika
Mashariki, Afrika na Dunia nzima .
 

Mjadala ni kuhusu kipimo cha utendaji wake unaochukua
nafasi pana katika vichwa vya  Magazeti ya nje na ndani, kwenye vipindi
vya runinga na mitandao ya kijamii,  Kitaifa na Kimataifa yote ikiwa ni
katika kuutazama uadilifu wake, uwazi na  uwajibikaji wa Serikali yake
chini ya misingi  ya uzalendo.
 

Watu mbalimbali wamekuwa wakijadili kutokana na
kushawishika kwao Rais Magufuli kuhusu umakini alionao, uchungu kwa nchi
yake na watu anaowaongoza akiwa na azma ya kupigania na kutetea maslahi
ya umma huku akitaka rasilimali za nchi kuinufaisha nchi na watu. 

Hakuna mtu au kiongozi  wa ndani au nje ya  chama tawala na
nje ya nchi waliotumwa wajadili wanavyojadili iwe kwa kumpongeza na
kumsifu kunakofanywa na watu hao.  

*Ndugu Waandishi wa Habari*

Waswahili wa kale na wahenga wana semi mashuhuri
isemayo“Kizuri hujiuuza na kibaya Hujitembeza”. Yaonekana ndivyo
inavyotokea kwa walimwengu wanavyoutazama na kuufuatilia uongozi wa
Awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli na Serikali yake katika
mtazamo chanya wenye  mafanikio. 
 

Alichokisema Mzee Mwinyi si kuwataka au kuwashawishi
wananchi kufanya mabadiliko ya Katiba hatimaye kumpa nafasi ya vipindi
vingine vya utawala Rais John Magufuli abaki madarakani kinyume na
matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Matamshi ya Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliyaweka bayana
akiyatanguliza  utangulizi wa maneno adhimu na dibaji yaliosema
nanukuulaiti nchi yetu isingelikuwa si yenye kufuata  utawala wa
kikatiba, Rais Dk John Magufuli alitosha na kufaa  kuongoza nchi yetu
kwa siku na miaka mingine.

Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM) hatuoni kama hilo ni kosa au
baa, ama iwe mwao au uonekane  uchuro kutokana na maneno hayo. Mzee Ali
Hassan Mwinyi ni mweledi, mlinzi mzuri wa Demokrasia na mtu anaheshimu
Katiba, Katu hakusema na kutaka Katiba ibadilishwe ili Rais abaki
madarakani kama inavyopotoshwa kauli yake.
 

Ndugu Waandishi wa Habari

Hata hivyo inaonyesha wanaojiita Wazee wa CHADEMA hawana
kumbukumbu ya kutosha. Wamesahau   Rais wa Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa
marehemu  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitawala kwa kipindi cha
miaka 23 tokea mwaka 1961 hadi mwaka 1985. 

Mwalimu Nyerere hakutawala miaka 23 kwa lazima yake, nguvu
za udikteta au kutumia misuli ya ubabe, alitawala  kwa matakwa, ridhaa,
utashi na maamuzi ya wana nchi wenyewe  ndiyo waliomshinikiza na
kumuomba kila wakati abaki madarakani kila alipopania kujiuzulu na
kumpisha mtu mwingine. 

Ifahakime kuwa Nchi yoyote na mahali popote, dunia
inahitaji ipate mtawala na utawala wenye tija, manufaa na maendeleo
yanayoonekana, kuwaridhisha au kuwapendezesha na kuwanufaisha wananchi.
 

Kushawishika na kuhamasika kwa wananchi na watu mbali mbali
juu ya kazi nzuri inayofanywa na Dkt. Magufuli nadhani imewakumba mpaka
Viongozi wenye nyadhifa mbali mbali katika Vyama Vya Siasa na makundi
mengine. Mfano siku za karibuni  kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi na
wanachama wa Chadema wakiwemo madiwani sita kwa hiari na ridhaa yao
wameamua kuachia ngazi na kukikimbia Chadema wakirejea CCM kwa
kuridhika, kutosheka na utendaji wa Serikali ya Rais Dk John Magufuli. 

Wanaojiita Wazee wa Chadema ingelipendeza sana kama
wangekuwa na mapenzi na chama hicho wangalikaa chini kutafakari na
kutathmini sababu ipi inayowafanya wanachama, viongozi waandamizi  na
madiwani hasa katika Mkoa wa Arusha wakikimbie chama hicho na kurejea
CCM badala ya wazee hao kucheza ngoma isiowahusu.
 

Ndugu Waandishi wa habari

Wote hapa tunaelewa Katiba ya nchi si Quran wala Bibilia.
Katiba imetungwa kutokana na maoni, weledi na utashi wa watu. Na watu
hao hao kwa kujali  kwao mahitaji na matakwa yao,  wanaweza kugeuza
chochote ndani ya katiba kwa kujali maslahi yao na wala  isiwe baa au
muujiza.

Umoja wa Vijana wa CCM unaamini ukishafikia hatua ya uzee
wakati mwingine unapoteza kumbukumbu muhimu, tunawakumbusha wanaojiita
wazee wa CHADEMA hakuna ushahidi  unaoonyesha  Mzee Mwinyi aliwahi kuwa
na mpango wa kutaka kujiongezea muda ili abaki madarakani kama
ilivyodaiwa na genge la Wazee hao. Kama mjuavyo kule Chadema kuna
maprofesa wa kuzua hili nalo Mzee Mwinyi wamemzulia na kumpakazia. 

Ingalikuwa Mzee Mwinyi alitamani kujiongezea muda ili
aendelee kubaki madarakani kwa wakati ule, angeweza kwa sababu uongozi
wake uliwakuna na kuwapendezesha mno wananchi mijini na vijijini na wala
isingelikuwa ni kazi kubwa ya kukubalika na kuungwa mkono . 

Zipo semi na hadithi nyingi zinazodai Mwalimu Nyerere
katika Kitabu chake cha Tanzania na Hatma ya Uongozi alikiandika kwa
lengo la kuwalenga viongozi  aliowakusudia kuwapasha na kutaka
wajisahihishe, kujisuta, kujiuzulu au kujirejebisha.

Ukweli ulivyo  si hivyo, Mwalimu kama Mwalimu
kitaaluma  aliandikia Kitabu chake kwa msukumo wa maono yake ili kuiasa
nchi yetu, viongozi wa sasa na wajao pia kuitazama hatma ya nchi yetu
kiutawala, kidemokrasia na kiutendaji bila kumlenga au kumdhamiria
yeyote kama inavyodaiwa na makuhani wa kuzua.
 

Ndugu zangu Waandishi wa habari.

Mtu mwerevu siku zote  anapotaka kumuasa mwenzake atoe
kibanzi katika jicho lake, kwanza huanza kutoa yeye boriti katika jicho
lake. Kama tujuavyo Katiba za baadhi za vyama vya Siasa vikiwemo vile
vya Ukawa. Katiba zao zinalalamikiwa kwa madai ya kuwa na udikteta. 

Tumeshuhudia mivutano ikirindima  ndani ya vyama hivyo huku
viongozi wa Vyama hivyo wakigombana kwa sababu ya kulinda matakwa ya
Katiba zao na baadhi yao wamekuwa ni zaidi ya wafalme na masultani
waliojenga  himaya ndani ya Vyama vyao huku wakiwa hawana ndoto wala
fikara ya kuachia madaraka.

Wapo wanachama wengine wamefukuzwa na hata kuvuliwa
uanachama ndani ya vyama vya upinzani kwasababu  ya kutaka kuwania
nyadhifa za juu ambazo wakubwa hawataki ziguswe kwakuwa kushika nafasi
hizo  ni kunagusa maslahi yao.

Wengine wanadaiwa kupoteza maisha katika mazingira ya
kutatatanishi kwa kujaribu kwao kuchukua fomu za kuwania nafasi za juu
huku wagombea urais wengine waliohama toka vyama vingine walipojiunga na
vyama hivyo nyakati za asubuhi, jioni yake wakapitishwa kwa mbwembwe
kuwa wagombea urais kinyume na matakwa ya Katiba zao . 
 

Ndugu Waandishi wa Habari

Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM  tunawataka wazee maslahi wa
Chadema waache kulishwa maneno na kuwa wazushi na waongo, waache papara
ya kujibu kila wanachokisikia kwa kuchochewa na ushabiki baada ya
kuoayiwa milungula na bahashish na kukimbilia  kuwadhalilisha viongozi
waliolitumikia Taifa hili kwa uadilifu na bidii na juhudi huku
wakiongoza nchi kwa  hekima, busara   kubwa zilizosaidia kuleta mageuzi
kadhaa  ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yalioacha alama ya utumishi wao
uliotukuka kwa watanzania. 

Tunaendelea kuwaaminisha watanzania Chama Cha Mpainduzi ni
chama kikubwa ndani Afrika na duniani kwa ujumla hivyo siku zote
hakifanyi makosa katika kuwaletea viongozi makini, wenye upeo na uweledi
wa hali ya juu.

Ahsanteni

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU

No comments :

Post a Comment