Kwa hisani ya http://www.malunde.com/2017/06/mhadhiri
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Tamisemi), George Simbachawene amemteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM), Profesa Davis Mwamfupe kuwa diwani katika Manispaa ya
Dodoma.
Juzi Mkurugenzi wa Manispaa ya
Dodoma Godwin Kunambi alimtaja Profesa Mwamfupe pamoja na wenzake wawili
Roze Nitwa (CCM) na Vicent Tibalindwa (Chadema) kuwa waliteuliwa na
Waziri kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.
Kunambi alisema Simbachawene
aliteua majina sita kwa vyama vya Chadema na CCM ndipo wakayapigia kura
likiwamo jina la Mwamfupe aliyetokea CCM.
“Waziri alitumia sheria namba
288 (24) (2d) ya Serikali za mitaa na kanuni za uteuzi za mwaka 2010
sura ya 4 (1) na 5 (1) vinavyompa mamlaka ya kufanya hivyo bila kuulizwa
na humteua mtu ambaye ni mkazi wa eneo husika,” alisema Kunambi.
Manispaa ya Dodoma haina Meya
baada ya Jaffary Mwanyemba kuondolewa na madiwani Machi mwaka huu kwa
madai ya matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo
alikana madai ya kumwandaa msomi huo wa uchumi katika nafasi ya Umeya
ingawa alisema kila mtu mwenye sifa za kuwa diwani ana haki ya kugombea
nafasi ya uongozi ikiwamo meya.
Mkurugenzi huyo aliwaondoa hofu
waliokuwa wamejenga nyumba zao katika maeneo ambayo hayajapimwa kabla
ya kuvunjwa kwa CDA akisema hawatasumbuliwa badala yake watarasimishwa
huku akitoa tahadhari kwa wavamizi wa maeneo na viwanja kuwa lazima
watavunjiwa.
Naibu Meya wa Manispaa ya
Dodoma, Jumanne Ngede alisema baraza la madiwani halina shaka na uteuzi
huo na kwamba watapewa ushirikiano katika kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ikiwamo mchakato wa makao makuu.
Alisema mpango uliopo katika
manispaa hiyo ni kujipanga kuwa na ugeni mkubwa ambao umeingia mkoani
hapo ikiwemo maofisa wa serikali.
Mmoja wa madiwani ambaye
hakupenda kutajwa jina lake alisema mpango wa uteuzi wa msomi huyo
unaweza kuwagawa madiwani kwani kuna kila dalili za kuandaliwa kushika
kiti hicho huku wengine wakitaka apewe nafasi katika kamati ya uchumi na
fedha tu ili akaonyeshe uzoefu wake huko.
No comments :
Post a Comment