Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Sheikh Nurdin Kishik ambaye ni Mhadhiri wa Kimataifa wa
Dini ya Kiislaam, (kulia) na ujumbe wake, ofisini kwake bungeni mjini
Dodoma Juni 2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza baada ya kushiriki katika sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa
Al- Gadaf mjini Dodoma Juni 2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili liendelee kudumu katika hali ya amani na utulivu.
Amesema suala la kudumisha amani
na utulivu ni jukumu la kila mmoja, hivyo kila
mwananchi kwa imani yake
ahakikishe anashiriki kutunza hali hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Ijumaa, Juni 2, 2017) baada ya kumaliza kuswali sala ya Ijumaa katika
Msikiti wa Al-Gadaf, mjini Dodoma.
Amesema ni vema kila mwananchi
akajivunia hali ya amani na utulivu iliyoko nchini kwa kuwa ndiyo
inayowezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
“Tuendelee kudumisha amani, tufanye ibada kila mtu kwa imani yake.
Serikali inaheshimu dini zote kwa sababu ndizo zinazojenga amani na
mshikamano,” amesema.
Pia amewataka wazazi wahakikishe
wanawalea watoto wao katika mazingira ya kidini ili wanapokuwa watu
wazima waje kuwa raia wema. “Tuendelee kuhamasisha watoto wetu
wasikilize mahubiri ya dini; ni jukumu letu sisi kama wazazi kuwahimiza
wahudhurie mahubiri ya viongozi wa dini ili waweze kujijenga vyema
kimaadili na kiimani pia.”
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewakumbusha Waislamu wahakikishe wanautumia vizuri mwezi mtukufu
wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na kusaidia watu wenye mahitaji. “Leo ni
Ijumaa ya kwanza katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, nawaomba
tutumie vizuri mwezi huu ili tupate baraka,” amesema.
Ibada hiyo ya sala ya Ijumaa
iliongozwa na Sheikh Nurdin Kishki ambaye ni Imamu wa Msikiti wa
Vetenari, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Kishki katika hotuba yake,
aliwasisitiza Waislamu waendelee kufanya mambo mema yenye kumpendeza
Mwenyezi Mungu ikiwemo kuwatunza wazazi wao, kumswalia Mtume Mohammed
(S.A.W) na kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
No comments :
Post a Comment