Tuesday, May 30, 2017

WCF YAWATAKA WAAJIRI KUTII SHERIA BILA SHURUTI


unnamed
Mjumbe wa  Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi  (WCF)  Richard Wambali akifungua Semina ya uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na mfanyakazi jijini Dar es Salaam leo (jana).
2
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Laura Kunenge akichangia mada katika semina ya uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na mfanyakazi jijini Dar es Salaam leo (jana).
4
 Mwanasheria Mwandamizi Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi  (WCF) Deogratius Ngowi  akitoa mada katika Semina ya uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na mfanyakazi jijini Dar es Salaam leo (jana).
5
Baadhi ya washiriki wa semina ya uelimishaji kwa waajiri wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi wa semina hiyo ambaye ni Mjumbe  wa Bodi ya  Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Richard Wambali (Picha Zote na Benjamin Sawe)
…………………………….
                                                  NA BENJAMIN SAWE
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), umeendesha semina ya siku moja kwa waajiri nchini ili kutoa elimu juu ya shughuli za Mfuko na wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi wao katika kujisajili na ...kuwalipa michango kwa niaba ya waajiriwa wao.
Akizungumza katika semina hiyo Mjumbe wa Bodi ya Mfuko huo Richard Wambali amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kumekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda hivyo kupelekea ongezeko la wafanyakazi ambapo chombo hicho ndio mkombozi wa majanga yatokanayo na kazi.                
“Ni muda muafaka kwa waajiri kutambua wajibu wenu katika Mfuko huu na pia kutambua madhara ya kutotekeleza wajibu wenu” Alisema Bw. Wambali.
Alisema Mfuko huo ulioanzishwa kwa sheria ya bunge namba 20 kifungu cha 5 ya mwaka 2008, una madhumuni ya kutoa fidia kwa Wafanyakazi kutokana na ulemavu au vifo viinavyosababishwa na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na kukuza mbinu za kuzuia matukio ya ajali.
Katika hotuba yake, Bw Wambali alieleza umuhimu wa waajiri kuwalipia michango wafanyakazi wake kama sheria inavyotaka, ili kuwawekea akiba pindi wapatapo na majanga wakiwa kazini.
Mfuko huo ambao umeanza kazi rasmi Julai 1, 2015, lengo kuu ni kutekeleza nia ya Serikali kukabiliana na changamoto za ulipaji wa fidia kwa Wafanyakazi katika mfumo wa utoaji fidia uliokuwepo awali
Bw.Wambali  alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kiwango kidogo cha malipo ya fidia(kiwango kisichozidi shilingi 180,000) kwa ulemavu wa kudumu na shilingi 83,000 kwa wategemezi endapo kifo kitatokea kwa Mfanyakazi husika.
Akinukuu sheria iliyoanzisha Mfuko huo, Bw. Wambali alisema, kifungu cha pili (2), cha sheria ya fidia kwa wafanyakazi namba 20/2008 cha mfuko huo unawahusu Waajiri na Wafanyakazi wote katika sekta ya Umma na Binafsi, Tanzania Bara pekee.
“Naomba ieleweke, anayepaswa kuchangia kwa mujibu wa sheria hii ni Mwajiri na sio mfanyakazi kukatwa mshahara wake.” Alifafanua Bw. Wambali.
Akizungumza wakati akitoa mada Afisa Matekelezo Bw. Musa Mwambujule amesema, Mfuko umeamua kuandaa semina hiyo ili kutoa elimu zaidi kwa waajiri  kwa kutambua kuwa waajiri ndio wadau wakuu wa Mfuko huo na semina hiyo itawasaidia kujua kazi za Mfuko lakini pia wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi katika kutoa michango ya kila mwezi.
Nae, Mwanasheria wa Mfuko huo Bw. Deogratius Ngowi, alisema, Mfuko huo upo kisheria ili kutoa fidia kwa wafanyakazi watakaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na umeundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi Sura ya 263 iliyorejewa Desemba, Mwaka 2015.

No comments :

Post a Comment