WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AFUNGUA KUTANO WA ROTARY CLUB ARUSHA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akivishwa beji ya uanachama wa Rotary Club na Dk. Manoj Desai kwenye
mkutano wa 92 wa mwaka unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District
9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa
kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Rotary Club kwenye mkutano wa 92
wa mwaka unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika
ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akifungua mkutano wa 92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda
na Tanzania (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4,
2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Washiriki wa Mkutano mkutano wa
92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District
9211) wakishangilia mara baada ya Waziri Mkuu kutangaza kuwa yeye na mke
wake, Mary Majaliwa wanajiunga na Rotary Club katika ukumbi wa AICC
jijini Arusha Mei 4, 2017.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Awa mwanachama wa 651 kujiunga na klabu hiyo, mkewe pia ajiunga
*Aaahidi kushawishi viongozi wa Serikali na wabunge wajiunge kwa wingi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameutaka uongozi wa Klabu ya Rotary nchini uangalie uwezekano wa
kuisaidia Serikali kupambana na ugonjwa wa Malaria.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye leo
hii (Alhamisi, Mei 4, 2017) amekuwa mwanachana wa 651 kujiunga na klabu
hiyo, ametoa wito huo wakati akifungua mkutano wa 92 wa mwaka wa
Rotary
unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika ukumbi
wa AICC jijini Arusha.
“Ninatambua kazi nzuri
inayofanywa na Rotary Club katika kuisaidia jamii kwa vile na mimi
mwenyewe nimekuwa nikisaidia jamii. Kwa hiyo mimi na mke wangu Mary
Majaliwa tunajiunga tukiwa ni wanachama wa 651 na 652 ili kuongeza nguvu
ya Rotary kusaidia jamii,” alisema huku akishangiliwa na washiriki
zaidi ya 1,000 waliohudhuria mkutano huo kutoka
Uganda, Tanzania, India, New Zealand na Australia.
Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa
klabu hiyo uongeze mikakati ya kutangaza kazi wanazozifanya ili kuondoa
dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kwamba wanaojiunga na klabu
hiyo ni watu matajiri na watu maarufu.
“Kazi mnazozifanya ni kubwa na
nzuri mno kwa jamii. Lakini itabidi mjitangaze zaidi ili watu wengi
zaidi watambue kazi zenu na waweze kuwaunga mkono,” alisema.
Waziri Mkuu aliahidi kuwashawishi
viongozi wengine wa Serikali, taasisi za umma pamoja na Wabunge
wajiunge kwa wingi na klabu hiyo. Tanzania ina klabu za Rotary 36 zenye
wanachama 650 wakati Uganda ina klabu za Rotary 93 zenye wanachama
2,700. Tanzania na Uganda zinaunda District 9211 katika mfumo wa
kimataifa wa rotary.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kuwapongeza wana-Rotary kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusaidia jamii
hasa kwenye sekta za maji, elimu, na afya.
Alisema Rotary inatambulika
duniani kwa kampeni yake ya kutokomeza ugonjwa wa polio; na kupitia
michango ya wana-Rotary, Tanzania hivi sasa haina mgonjwa yeyote wa
polio.
“Licha ya uchache wenu, natambua
mchango mkubwa unaotolewa na Rotary Club hapa nchini. Hivi
karibuni, Rotary Club saba ziliungana na Benki M na kujenga hospitali
kubwa ya watoto pale Muhimbili (MNH) na Kituo cha Ujasiriamali kwa
Vijana pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),” alisema.
“Miradi mingine inayofadhiliwa na
Rotary Club ni ujenzi wa hospitali ya akinamama wajawazito mkoani
Dodoma, utoaji wa vitabu vya ziada 20,000 kwenye shule za sekondari
zaidi ya 40 mkoani Tanga pamoja na miradi ya maji safi kwenye wilaya za
Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake, District
Gavana wa Rotary 9211 ambaye anamaliza muda wake, Bw, Jayesh Asher
wana-Rotary duniani wanaamini kwamba Serikali za nchi mbalimbali
haziwezi kutekeleza majukumu yote kwa wananchi wake kwa hiyo wanajiunga
na kutoa rasilmali zao ili kusaidia jamii zenye uhitaji.
Akizungumzia kuhusu uchahe wa
wanachama hapa nchini, Bw. Asher alisema Rotary Club ya Uganda imepata
umaarufu kwa sababu viongozi wengi wamejiunga na klabu hiyo wakiwemo
Mawaziri, Spika wa Bunge la Uganda, wabunge na mabalozi.
“Hapa Tanzania itabidi
tutangaze zaidi kazi zetu ili tuweze kuwavuta viongozi wa kisiasa na wa
umma na pia kuongeza wanachama zaidi,” alisema.
Mkutano huo wa siku tatu, utamalizika Juni 6, mwaka huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 4, 2017.
No comments :
Post a Comment