Kumekuwepo
na taarifa iliyoandikwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Clouds
Media Group za Facebook na Instagram ikimnukuu Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam Dkt. Grace Magembe akisema kuwa ‘‘Upimaji wa VVU nyumba
kwa nyumba sasa rasmi, mchakato unaendelea na zoezi litaanza rasmi
mwishoni mwa mwezi huu“.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mara nyingine, inapenda kutoa ufafanuzi
kwamba UKIMWI HAUPIMWI NYUMBA KWA NYUMBA bali inafanya utafiti wa
Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania ambapo UKIMWI ni ugonjwa
mmojawapo unaopimwa katika utafiti huu. Aidha, utafiti huu unafanyika
kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze
kuwakilisha kaya nyingine ambazo hazihusiki moja kwa moja. Utafiti huu
unajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa
kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na unahusisha
watu wazima wasiopungua 40,000 na watoto takribani 8,000.
Kwa Dar es Salaam, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI utahusisha kaya zisizozidi 1,000
kati ya kaya 1,000,000 na unatarajia kuanza tarehe 31 Mei, 2017 na kuendelea kwa wiki zisizozidi tatu (3).
Mbali
na upimaji wa UKIMWI, utafiti huu pia unapima kiwango cha maambukizi ya
Kaswende, Homa ya ini (Hepatitis B), uwepo wa viashiria vya usugu wa
dawa, maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa watu
wanaoishi na VVU (Viral load), wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa
rika zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell
count). Aidha, kupima ni hiari na watakaogundulika kuwa na maambukizi,
watapata rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu bure katika vituo vya kutolea
huduma za afya.
Ifahamike
kwamba, utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17
unafanyika nchini kwa mara ya nne (4) ambapo utafiti wa kwanza
ulifanyika mwaka 2003, wa pili mwaka 2007 na wa tatu mwaka 2011.
Hivyo, NBS inapenda kuwatoa hofu Wananchi kuwa, kufanyika kwa utafiti
huu sio jambo jipya na Watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti
huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90 na mpaka sasa
utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na kwa
upande wa Tanzania Zanzibar, utafiti huu umekamilika katika maeneo yote
yaliyochaguliwa.
Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendelea kufanyika nchini,
ukisimamiwa na NBS kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa
Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS),
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar
(ZAC).
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),
DAR ES SALAAM.
03 Mei, 2017
No comments :
Post a Comment