Tuesday, May 30, 2017

BENKI KUU YATOA MAFUNZO YA NOTI HALALI KWA WATUMISHI WA OFISI YA MKUU WA MKOA SINGIDA.


2
Mwangalizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida Khadija Hamisi na Mkaguzi wa ndani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Alfred Kalama wakisikiliza kwa umakini alama zinazopatika katika noti halali wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.
unnamed
Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Justo Herman akikagua noti halali wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.
1
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango na Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida Florian Kimoro wakionyeshana alama za noti halali wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.
3
 Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida George Kulwa akitoa shukrani kwa niaba ya watumishi wote waliopata mafunzo ya Benki kuu ya Tanzania.
4
 Maafisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania Rehema Zongo na Rajab Ibrahimu wakisikiliza maswali na kutoa ufafanuzi kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mara baada ya kutoa mafunzo ya alama za noti halali.
5
 Maafisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania Rehema Zongo na Rajab Ibrahimu wakisikiliza maswali na kutoa ufafanuzi kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mara baada ya kutoa mafunzo ya alama za noti halali.
……………………
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa mafunzo kwa watumishi wote wa ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Singida juu ya alama zinazopatikana katika noti halali za fedha ya Tanzania leo asubuhi katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akitoa mafunzo hayo Afisa Kutoka Benki Kuu ya Tanzania Rehema Zongo amewafafanulia watumishi hao namna ya kutambua noti halali kwa vitendo huku akisisitiza alama muhimu zinazopatikana katika noti halali ili waweze kutofautisha na zile bandia.
Zongo amesema watumishi wanatakiwa kuichunguza noti halali, waipapase ili kuhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalumu mfano maandishi yanayoeleza fedha halali kwa malipo ya shilingi mia tano, elfu moja, elfu mbili, elfu tano na elfu kumi.
Amewasisitizia kuwa wanaweza kuitambua noti halali kwa kuangalia sura ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayoonekana unapoimulika noti kwenye mwanga na pia kukagua utepe maalumu kwenye noti za shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 unaoonekana kama madirisha yenye umbo la almasi ambapo hubadilika badilika noti inapogeuzwa geuzwa.
Zongo ameongeza kuwa watumishi na wananchi wote wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kuwa noti bandia zipo mtaani na kuwa hazina thamani yoyote.
“Ukipata noti bandia au hata kama unaishuku ni bandia, ipeleke benki au kituo chochote cha polisi kilichopo karibu nawe, lakini pia tuwe na utaratibu wa kuthibitisha uhalali wa noti mara uzipatazo kwa kuzingatia alama tulizowafunzisha leo, na pia tunaomba muwe waalimu kwa kuwafundisha wengine alama hizo”, amesema Zongo.
Amesisitiza kuwa kugushi pamoja na kumiliki fedha bandia kwa nia ya kuzitumia ni kosa la jinai linalosababisha mhusika kushitakiwa kwenye vyombo vya sheria hivyo wanapaswa kuwa makini, kutoa taarifa sahihi na katika sehemu husika, pia kuwa na utaratibu wa kuchunguza noti.
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida George Kulwa kwa niaba ya watumishi wote waliopata mafunzo hayo ameishukuru Benki kuu ya Tanzania kwa kutoa mafunzo hayo.
George amesema elimu iliyotolewa kwa watumishi hao ni muhimu na itawasaidia si watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa pekee bali wananchi wote kwa ujumla kwakuwa watumishi hao watakuwa mabalozi wa elimu hiyo.
Aidha ameiomba benki kuu kuendelea kutoa elimu hiyo mpaka ngazi za vijiji ili taifa lote liwe na elimu sahihi na ya kutosha juu ya alama za noti halali huku akiwakaribisha tena katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kila mara wanapotaka kutoa elimu yoyote juu ya masuala ya fedha na uchumi wa Tanzania.

No comments :

Post a Comment