NA HUSNA SAIDI-
MAELEZO
TAKRIBANI shilingi
milioni 271 zinadaiwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoani Mara ikiwa
ni kodi ya Pango la Ardhi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipofanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya
ardhi hivi karibuni Mkoani humo.
Waziri Lukuvi alisema
kuwa amekagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini ili kuhakikisha wamiliki
wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya hatua za kisheria
hazijafuata dhidi yao.
“Nimeagiza kesi za
madai ya kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze
kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali zao haraka”, alisema Lukuvi.
Aidha Waziri Lukuvi
alimtaka Afisa Ardhi wa Manispaa ya Musoma Bw.Joseph Kamonga kuwasilisha majina
ya wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa
ni pamoja na kupiga mnada majengo na mali zao kama wakikaidi kulipa kodi hiyo.
Kwa upande mwingine
Lukuvi alifanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa ya Musoma
na kuwapongeza viongozi na watendaji wa Manispaa hiyo kwa kuwa Manispaa ya
kwanza nchini kuweza kuzindua mpango huo kutumia kampuni za ndani katika
utekelezaji wa mpango huo.
Kufuatia hatua hiyo
Waziri Lukuvi amezitaka Manispaa nyingine kutumia kampuni za ndani ya nchi
ambazo zimesajiliwa na Wizara ya Ardhi katika kutekeleza mipango
mbalimbali ya ulipaji kodi za ardhi.
Pia Waziri Lukuvi
aliiagiza Manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango
kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani na kutoa
nakala za kutosha ili mpango huo uwafikie wadau wote na kutaka mpango huo
utafsiriwe kwa Kiswahili ili Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waweze
kuwafikishia wananchi kwa urahisi.
No comments :
Post a Comment