Shirika lisilokua la Kiserikali
la Plan International limewawezesha jumla ya vijana 7356 wanaoishi
katika mazingira magumu kwa kuwapatia mafunzo ya Ufundi na Stadi za
maisha ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.
Takwimu hizo zimebainishwa na
Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE), Simon Ndembeka
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu idadi ya vijana
waliopangwa kufikiwa na mradi huo wa miaka mitatu unaotegemewa kuisha
mwaka 2018.
Ndembeka amesema kuwa mradi huo
wa miaka mitatu ulioanza tangu mwaka 2015, unatekelezwa kwa ushirikiano
wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya
Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya
ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na umepanga kuwafikia kwa awamu
jumla ya vijana 9100.
“Mradi huu umepanga kuwafikia
vijana 9100, kati yao wasichana ni asilimia 53, wavulana asilimia 37
pamoja na asilimia 10 kwa ajili ya vijana wenye ulemavu hivyo mpaka sasa
mradi unavyokaribia ukingoni tumeweza kuwafikia vijana 7356, tunaamini
tutawafikia vijana wote waliopangwa na mradi ifikapo mwaka 2018,”
alisema Ndembeka.
Ameongeza kuwa mradi huo umekuwa
na mafanikio makubwa kwani umewawezesha vijana wengi kujikomboa kwa
kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na fani walizozisomea
chini ya mradi hasa wasichana kwani wengi wao wamekuwa wakipewa mimba
na baadae kutelekezwa wakiwa hawana mahali pa kutegemea.
Kwa upande mwingine, Ndembeka
amesema kwa sasa jamii imetambua kuwa vijana wenye ulemavu wanaweza
wakafanya jambo kama wakiaminiwa na kuwezeshwa hivyo shirika limepata
mafanikio katika kuwawezesha vijana wenye ulemavu ili waweze kujitegemea
na kuwasaidia wengine.
Meneja huyo amezitaja baadhi ya
changamoto hizo kuwa ni upatikanaji wa vijana wenye ulemavu kwa sababu
sio jamii nzima inaelewa kuwa walemavu wanaweza wakafanya kazi hivyo
wanaamua kuwaficha ndani tabia ambayo inatakiwa kukomeshwa kwa nguvu
zote.
Kwa upande wake, mmoja wa
wanafunzi waliomaliza mafunzo ya mapishi chini ya mradi huo, Janeth
Thadeo amelishukuru shirika hilo kwa kuanzisha mradi ambao unawasaidia
vijana kama yeye kujiajiri na kupata fedha zinazomuwezesha kuhudumia
familia yake.
“Malengo yangu ya baadae ni
kuwatafuta vijana wenzangu kuwafundisha mafunzo ya upishi niliyoyapata
chuo cha VETA chini ya Mradi wa YEE ili kwa pamoja tuweze kufungua
sehemu kubwa ya biashara ya chakula itakayotupatia fedha zaidi”.alisema
Janeth.
Mikoa iliyopata fursa ya mradi wa YEE kutekelezwa ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara na Lindi.
No comments :
Post a Comment