Na Judith Mhina-MAELEZO
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ulikuja hapa duniani Aprili 13, 1922 kupitia kwa Mpendwa Marehemu Bibi
Mgaya wa Buritho kama zawadi kwa nchi ya Tanzania.
Mwalimu tunamshukuru Mungu kwa kutupa wewe ambaye umeitendea mambo makubwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
Mwalimu wakati nakumbuka kuzaliwa
kwako nimepata fursa ya kuangalia kazi ulizozifanya
mara baada ya
kuacha madaraka ya Urais na kujikita katika kazi kuu tano; Mosi pamoja
na kubaki na kofia moja ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya
kuimarisha Chama na alianza maandalizi ya kukabidhi Uenyekiti huo kwa
Rais aliyepokea madaraka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye
alikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Pili, mwaka 1986 baadhi ya
Viongozi wa nchi za Kusini mwa Dunia, walikuomba kuanzisha Tume ya
Uchambuzi wa maendeleo ya nchi za Kusini tangu miaka 30 iliyopita na
kuweza kuona hatua za maendeleo na changamoto zilizopo katika mataifa
hayo na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha ustawi wa wananchi.
Mwalimu Nyerere alikubali jukumu
hilo, ndipo alianza kutembelea nchi 19 katika Bara la Asia na Marekani
ya Kusini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu hayo mapya. Safari
ya kutafuta maoni hayo ilikuwa ni pamoja na kupata uthibitisho wa
kuwaelewesha wananchi na nchi hizo kuhusu majukumu ya Tume na aina ya
maoni yanayokusanywa.
Kazi hiyo aliifanya kwa miaka
mitatu na kutoa ripoti kuwa nchi za Kusini zifanye maendeleo yao yenyewe
yalenge maslahi ya wananchi walio wengi kwa kielelezo kuwa ili nchi za
Afrika ziweze kupiga hatua za maendeleo ni vyema ziwe na mshikamano kama
zinahitaji kushindana na nchi za Kaskazini.
“Nchi za Kusini zishirikiane
kibiashara, kwa kuwa nchi za Kusini zina mazoea ya kufanya biashara na
nchi za Kaskazini lakini hakuna utaratibu mzuri wa nchi za Kusini
kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe, au hata katika uwekezaji
rasilimali” alisema Mwalimu Nyerere.
Aidha, Mwalimu Nyerere alisema
Wataalam wengi wako Kusini lakini nchi za Kusini zinatafuta wataalam
kutoka Kaskazini, hivyo ni wajibu wa nchi za Kusini kujenga na
kuimarisha ushirikiano wa pamoja baina yao.
Tatu, Mwalimu alianzisha kituo
cha muda cha Nchi za Kusini pale Geneva ambapo Mwalimu na Viongozi
wengine walifanya kazi kwa muda wa miaka miwili, jukumu lao likawa
kuelezea shughuli za maamuzi na mapendekezo ya Tume.
Nne, kuanzisha Ofisi ya kudumu ya
Nchi za Kusini pale Geneva kwa ajili ya Mataifa hayo kutoa hoja kupitia
vuguvugu la nchi za kundi la 77 ambazo hazikuwa na chombo cha
kuwasaidia kupaza sauti zao.
Mwalimu akapokea jukumu hilo na
kuanzisha Ofisi ya kudumu ambayo ilikuwa chombo cha Serikali badala ya
chombo cha kiraia na kuhusisha nchi 49 ambazo ziliweka sahihi, pamoja na
nchi kubwa ulimwenguni ikiwemo India, Brazil na Afrika ya kusini.
Tano, alikuja na wazo la
kuanzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere, hatua iliyotokana na harakati za
kazi yake ya kuunganisha nchi za kusini, ambapo alitaka taasisi hiyo
kufanya kazi zake katika ukanda wote wa nchi za Bara la Afrika.
Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kuangalia maendeleo ya watu, kupitia dhana ya umoja na ushirikiano miongoni mwao.
Nakumbuka hotuba ya Mwalimu Nyerere aliitoa mwezi Februari mwaka 1960, akiwa Rais wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) , alikaribishwa
nchini Marekani katika Kongamano la Afrika katika Chuo cha Wellesley
Massachusetts kuongelea kuhusu “Nafasi ya Afrika Duniani” .
Katika hotuba hiyo, Mwalimu
alizungumzia hatua mbalimbali za ukombozi wa Bara la Afrika, mchango wa
Waafrika katika Mataifa ya Ulaya na Marekani. Mwalimu alilisemea Bara la
Afrika Kama Bara la matumaini kwa ubaguzi wa rangi.
Mwalimu alisisistiza kwa kusema
“Muda utafika ambapo Marekani na Ulaya Magharibi watajisikia vibaya
jinsi walivyoitumia Afrika” huku akitolea mifano ya mateso na manyanyaso
waliyoyapata Waafrika ikiwemo vita vya Mau Mau nchini Kenya, vifo vya
watu wa kabila la Waherero nchini Namibia, vita vya Majimaji nchini
Tanzania.
Hotuba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa
Mwalimu Nyerere kuchapishwa kimataifa, hakika imeonyesha kwa dhati,
Mwalimu hata kabla ya Uhuru alitambua nafasi ya umoja katika kupigania
uhuru wa Bara la Afrika.
Aidha, ndoto hii ya umoja
alisafiri nayo katika kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nafasi
ya Uenyekiti Jumuiya wa Nchi zilizo mstari wa mbele katika Ukombozi
Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nyingine nyingi.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere
dhumuni lake kuu ni kuendeleza Amani, Umoja na Utulivu wa Maendeleo ya
pamoja Barani Afrika. Mwalimu alikuwa muanzilishi na Mweneyekiti wa
kwanza wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Septemba 14, 1996 alikaribishwa
Kilimanjaro hoteli kuhutubia na kuzindua Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Umuhimu wa Umoja, umuhimu wa ukubwa wa soko, Amani baina ya nchi ndani
na nje ya nchi na Maendeleo katika Afrika.
Alipata fursa ya kukutana na
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaeleza juu ya Taasisi
hiyo na madhumuni yake. Katika kipindi hiki Mwalimu alikuwa msuluhishi
wa mgogoro wa Burundi.
Mwalimu leo ungetimiza miaka 95
tangu kuzaliwa, kimwili hatupo pamoja nawe, lakini fikra zako, mitazamo
yako, utendaji wako bado ni dira na muelekeo wa Taifa letu Daima
tutazifuata. Hakika siku ya leo ni siku muhimu sana kwa nchi yetu. Mungu
ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika
No comments :
Post a Comment