NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa
Magharibi Unguja kimesema kina matarajio ya kufanyika kwa ufanisi
uchaguzi wa Chama na jumuiya ndani mkoa huo baada ya kuzipatia ufumbuzi
changamoto zilizojitokeza katika mchakato huo hivi karibuni.
Akizungumza Katibu wa Mkoa huo,
Bi. Aziza Ramadhan Mapuri mara baada ya kufanya ziara fupi katika
Wilaya za Dimani na Mfenesini na kuzungumza na wajumbe wa Kamati za
Sekreterieti za wilaya 6hiyo kwa lengo la kufanya tathimini ndogo juu ya
maendeleo na kasoro zilizopo katika uchaguzi huo.
Amesema ziara hiyo imekuja baada
ya wanachama kutojitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi kwa
ngazi za mashina na matawi ya jumuiya kutokana na kuwa na hofu
iliyotokana na kutoelewa marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, juu
ya kipengele cha kinachosema kazi za muda wote kwa baadhi ya nafasi
zinazogombewa.
Alisema wanachama wengi waliokuwa
na nia ya kuchukua fomu walitawaliwa na hofu ya kuwa endapo
watajitokeza kuwania nafasi za ngazi hizo watakuwa hawana fursa za
kugombea nafasi zingine katika ngazi za juu.
Aidha Katibu huyo alifafanua
kwamba nafasi zilizotajwa kuwa ni za muda wote ni zile za kiutendaji
zikiwemo za Katibu na Mwenyekiti lakini zingine zilizobaki zinaruhusiwa
kushika nafasi zaidi ya moja na kwa ngazi tofauti.
Pia alieleza kwamba chanzo cha
kuwepo kwa ziara hiyo ni baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.
Abdalla Juma Saadalla kubaini mapungufu katika mchato huo na kuagiza
ngazi husika za chama na jumuiya kutoa elimu na maelekezo ya kina juu ya
changamoto hizo kwa viongozi wa ngazi zote ili nao wawaelimishe
wanachama katika maeneo husika.
” Tunatarajia kuwa baada ya
kuongezwa muda wa uchaguzi wanachama wetu wengi watajitokeza zaidi
kuchukua fomu ili kupata viongozi wengi.”, alisema Bi. Aziza.
Hata hivyo alipongeza maamuzi ya
busara na hekima ya kujenga chama yaliyofikiwa na Naibu Katibu Mkuu huyo
kwa kuongeza muda wa uchukuaji wa fomu ambapo kwa mujibu wa taarifa ya
awali uchaguzi wa ngazi za chama ulikuwa ufanyike April 17 hadi 31 mwaka
huu lakini kwa sasa utafanyika April 25 hadi 31 mwaka huu.
Kwa upande wa uchaguzi huo kwa
ngazi ya Jumuiya za chama utafanyika Juni 18 hadi 22 mwaka, na matarajio
ya mkoa huo ni kuona muda uliobaki unatumiwa vizuri na Wanachama wa
chama hicho kwa kuchukua fomu kwa wingi ili kupata viongozi na watendaji
wenye sifa na vigezo vya kukiimarisha chama na jumuiya.
No comments :
Post a Comment