Wednesday, March 1, 2017

WAZIRI WA AFYA UMMY MWALIMU AINGIA OFISI YA DODOMA


images
=Katika kuitikia agizo la Serikali kuhamia Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu amefika kwenye Ofisi za Wizara yake iliyopo eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma, sehemu ya Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii na kukutana na watumishi wa Wizara yake.
Mhe. Ummy alipokelewa kwa shangwe na bashasha na watumishi  wa Wizara yake – Idara Kuu ya Afya na Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakiongozwa na
Katibu Mkuu wa Wizara Bibi Sihaba Nkinga. Waziri alipata muda wa kusalimiana na watumishi 106 waliotangulia kuhamia Dodoma katika Awamu ya kwanza ya Uhamisho na kujiridhisha na ari waliyonayo watuimishi.
Akiwa hapa UDOM, Waziri Ummy alitembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za matibabu ya kibigwa kwa wagonjwa zinapatikana kupitia Hospitali hiyo iliyoko eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma, ambayo imefungwa vifaa vya kisasa ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali yaliyoshidikana.
Akiongea na waandishi wa habari, Mhe. Waziri alifafanua kuwa katika kuhakikisha Serikali inasogeza huduma za afya kwa wananchi wake, wanafunzi na viongozi wanaohamia Dodoma, Hospitali ya Benjamini Mkapa imekamilisha kufunga vifaa vya kisasa vya matibabu ikiwa ni ‘MIR’ mashine ya ‘mamography’ inayotumika kuchunguza magonjwa ya saratani ya akinamama, na kwamba mashine hiyo inapatikana hapo hospitalini pekee hapa nchini.
Kufuatia kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa madaktari, wahuguzi na watumishi wa kada mbalimbali, Wizara itaangalia uwezekano wa kufanya uhamisho wa ndani ili kupunguza uhaba wa watumishi uliopo katika hospitali hiyo. Aidha, Wizara imeahidi kuwasiliana na Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kupata watumishi wakutosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watumishi.
Na Erasto T. Chingoro- Msemaji Kitengo cha Mawasilino Serikalini, WAMJJW

No comments :

Post a Comment