Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Tanzania inategemea kupata
Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja ya makubaliano
yaliyofikiwa baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa
Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari juu ya
makubaliano na mikataba ambayo
nchi za Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
“Tukitaka kujenga uchumi wa
viwanda ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu Ethiopia
wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie wataalamu
kutoka nchini kwake ili waje tuwaonyeshe maeneo mbalimbali watusaidie
katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme ambayo
yamesaidia sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini
kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa kupatikana kwa
umeme huo kutasaidia kuleta changamoto kwa shirika la umeme nchini
katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta ushindani katika
upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema kuwa wana mengi ya kujifunza
kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina historia inayofanana na
kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika kupata uzoefu
katika masuala mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kuja
nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili zinaweza kuunganisha
nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika eneo la ukanda wa
Afrika Mashariki na kati.
“Tanzania na Ethiopia ni nchi
ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio washindani bali tunasaidiana
katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika hatua mbalimbali za
kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini katika hatua zinazofanana,na huu
ni wakati muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu
wetu kwa ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.
Aidha amesema kuwa mabadiliko
ya kilimo katika nchi zetu ndio msingi wa maendeleo pamoja na
utumiaji wa teknolojia bora utasaidia katika maendeleo ya viwanda
vidogo vidogo.
Viongozi hawa wamekubaliana
kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali
zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na
gesi, elimu na mawasiliano.
Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Haile
Mariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza
kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa
thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
No comments :
Post a Comment