Wednesday, March 1, 2017

SSRA YAZINDUA MFUMO MPYA WA KURAHISISHA MAWASILIANO


kib1
Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Uhamasishaji cha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (Kulia), Sarah Msika akiwaelekeza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mfumo wa kupokea malalamiko kwa njia ya TEHAMA wakati wa mkutano na waandishi hao uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Kutoka kushoto ni Afisa TEHAMA wa Mamlaka hiyo, Ernest Masaka pamoja na Afisa Mwandamizi wa TEHAMA wa Mamlaka hiyo, David Ngh’ambi.
kib2 kib3
Afisa Mwandamizi wa TEHAMA wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), David Ngh’ambi akielezea jinsi ya kutuma malalamiko kwa njia ya simu wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam,kushoto ni Afisa TEHAMA wa Mamlaka hiyo, Ernest Masaka na kulia ni   Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Uhamasishaji cha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (Kulia), Sarah Msika.
……………………………………………………………………….
Na. Georgina Misama – MAELEZO
 
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imeanzisha mfumo wa TEHAMA utakaowawezesha wanachama kutuma na kufuatilia malalamiko yao moja kwa moja kwa mamlaka hiyo.
 
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo Cha Mahusiano na Uhamasishaji kutoka mamlaka hiyo Sarah Kibonde alisema Mfumo huo utaiwezesha SSRA kupokea na kushughulikia malalamiko ya wanachama moja kwa moja.
 
“Mfumo huu unapatikana katika simu za mkononi (mobile app), unapatikana kwa watumiaji wa simu za mkononi zinazotumia mfumo wa android na unatambuliwa kwa jina la SSRA” alisema Sarah.
 
Akitoa maelezo ya namna ya kutumia mfumo huo, Afisa TEHAMA wa SSRA Bw.Ernest Masaka alisema mara baada ya mwanachama kuingiza taarifa zake ambazo ni majina matatu, anwani ya posta, namba ya simu, pamoja na namba ya uanachama na makazi, mfumo utampa namba ya kumbukumbu ya lalamiko husika.
 
Aidha, taarifa hizi husaidia kumtambua muhusika na Mamlaka kufanya mawasiliano na mwanachama mwenye malalamiko pamoja na kushughulikia malalamiko husika moja kwa moja.
 
“Mfumo huu umeweka utaratibu wa mlalamikaji kufuatilia  hatua za utatuzi wa malalamiko yake kwa kumbukumbu za mlalamikaji” alisema Bw.Masaka.
 
Akizungumzia faida zinazopatikana kwa wanachama kutumia mfumo huo Bw.Masaka alisema ni pamoja uwekaji mzuri wa kumbukumbu kwa Mamlaka,kutoa mrejesho wa idadi na hatua za utekelezaji pamoja na mwanachama kupata mrejesho kwa haraka bila kujali mahali alipo ambayo itasaidia kupunguza ghara za fedha na muda.
 
Mamlaka inatoa wito kwa wanachama na wananchi wote kwa ujumla kutumia mfumo huu kwasababu unarahisisha mawasiliano kati ya mlalamikaji na Mamlaka.

No comments :

Post a Comment