WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli inautashi
wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezani na biashara nchini kwa
kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo amewakaribisha
wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja nchini.
Amesema Tanzania imefanya mageuzi
makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na
kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa
umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu amesema hayo jana
(Alhamisi, Machi 23,2017) wakati akifungua kongamano la Biashara na
Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lilifanyika katika Hotel ya
Labourdonnaise mjini Port Louis nchini Mauritius. Kongamano hilo
liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Alisema Tanzania ina uchumi imara
unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya
biashara bila ya kuingiliwa na Serikali, hivyo sekta binafsi imepewa
kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt.
Magufuli nawakaribisha kwa mikono miwili kuja na kuwekeza nchini
katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii na kutembelea
vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake na kwa
wafanyabiashara Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.
Alisema TIC na Mamlaka ya
Uwekezaji Zanzibar kwa pamoja vimeweka taratibu ambazo zinamwezesha
mwekezaji kupata mahitaji yake muhimu ya kuwekeza katika kituo kimoja
(One stop Centre).
Alibainisha baadhi ya mahitaji
hayo kuwa ni huduma za kusajili kampuni, kodi, uhamiaji, leseni za
biashara, ardhi pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji. Hali
ambayo inachangia Tanzania kupata wawekezaji wengi kutoka ndani na nje.
Waziri Mkuu alisema wawekezaji
wanaokuja kuwekeza Tanzania wanatoka katika mataifa mbalimbali kama
Marekani, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Autsralia, Umoja wa Falme za
Kiarabu (UAE) na hivi karibuni wanatarajia wawekezaji kutoka nchini
Mauritius.
“Ujio wa wawekezaji hawa haukuwa
wa bahati bali ni kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali
pamoja na suala zima la soko kubwa la bidhaa zao na huduma. Soko hili
linalozidi watu milioni 300 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika linatoa uhakika wa soko kubwa kwa mwekezaji yeyote anayekuja
Tanzania kuwekeza,”.
“Kuwekeza nchini Tanzania kunampa
fursa mwekezaji kupata fursa maalumu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki
(EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na soko la nchi ambazo
hazipakani na bahari. Nchi ambazo Tanzania ina mahusiano nazo mazuri ya
kibiashara ni Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo na Zambia.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika
kuheshimu wawekezaji Tanzania imesaini mikataba mbalimbali inayolenga
kuwalinda popote walipo kama Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA) na Africa Trade Insurance Agency.
Alisema Tanzania mbali ya hali ya
amani na utulivu wa kisiasa, pia imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa
rasilimali asilia ambazo zinatoa fursa nzuri kwa mwekezaji. “Hii ni
pamoja na ardhi yenye rutuba nzuri kwa kilimo, madini ya kila aina
kuanzia dhahabu, almasi, makaa ya mawe, tanzanites, chuma na gesi
asilia,”.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na
Waziri Mkuu wa Mauritius Mheshimiwa Pravind Kumar Jugnauth, Prime
Minister of the Republic of Mauritius; Waziri wa Mambo ya Nje wa
Mauritius Bw.
Seetanah Lutchmeenaaraidoo, Waziri
wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid
Salum Mohammed, Balozi wa Heshma wa Tanzania nchini Mauriutius Bw.
Cliford Tandali.
Wengine ni Mwenyekiti wa Taasisi
ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye,, Executive Director of
Tanzania Investiment Centre; Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Clifford
Tandar pamoja na Maofisa wa Serikali ya Tanzania na Mauritus
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MACHI 24, 2017.
No comments :
Post a Comment