Na Daudi Manongi-MAELEZO
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa
amewataka wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Mamlaka za
udhibiti kuwa wabunifu na kutumia fursa na rasilimali zilizopo
nchini
ili kuleta maendeleo chanya.
Amebainisha hayo leo Ikulu Jijini
Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kujadili nafasi ya Mashirika
ya Umma katika utekelezaji wa mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa
miaka mitano.
“Rai yangu leo ni kwamba kwenye
majadiliano yenu pendekezeni na kufanya mashirika ya umma yawe
endelevu,yapanuke zaidi na kuliongezea Taifa mapato na ndio maana
nafarijika sana kuona mkutano huu unajumuisha wadau wote muhimu ili
pamoja na kuweka mikakati ya namna mashirika ya umma ya Tanzania
yanavyoweza kushiriki kwenye utekelezaji wa mpango wa Maendeleo,”Alisema
Majaliwa.
Akielezea hali ya mashirika ya
umma nchini,Waziri Mkuu amesema kuwa utegemezi wa mashirika unaendelea
kupungua na mchango na gawio kutoka kwenye mashirika hayo unaendelea
kuongezeka na kuhimiza kuongezeka kwa ubunifu na matumizi mazuri ya
rasilimali chache zilizopo na kuongeza kati ya mashirika 65 ya
kibiashara,mashirika 8 yanaendeshwa kwa Ruzuku ya Serikali,wakati
mashirika 57 hayategemei ruzuku ya Serikali.
Ameagiza kuboreshwa kwa mwongozo
wa kupata wajumbe wa Bodi na kuwaagiza kuweka mwongozo rasmi wa namna ya
kupata wajumbe hawa kwani ni sehemu inayolalalmikiwa sana na wananchi.
Amesema kuwa wameyashirikisha
mashirika ya umma kwenye utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa sababu
vipaumbele vya mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano
ambayo ni ujenzi wa viwanda vya kuimarisha kasi ya ukuaji wa
uchumi,miradi mikubwa ya kielelezo na miradi wezeshi kwa maendeleo ya
viwanda ikiwemo barabara,reli,nishati,bandari maji na mawasiliano.
Aidha ameagiza kuondolewa kwa
urasimu katika shughuli za mashirika ya umma kwani unakwamisha
uboreshaji na maendeleo ya mashirika ya umma.
Waziri Mkuu pia ametoa rai kwa
viongozi wote wa mashirika ya umma kutosaini mikataba isiyo na tija kwa
Taifa ambayo inapelekea kupata hasara kubwa na kuhimiza mashirika haya
kushirikiana na mashirika ya nje pamoja na sekta binafsi ili kupata
nguvu ya pamoja katika kukuza uchumi.
“Ni lazima mashirika ya umma
yakafanya kazi kwa pamoja na kwa kushirikiana ikiwemo kubadilishana
mbinu na utaalamu ili kulifikisha Taifa hili katika azma yake ya kukuza
Uchumi wa viwanda kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu”,Alisisitiza
Mh.Majaliwa.
No comments :
Post a Comment