Maadhimisho
ya siku ya Kifua Kikuu Duniani “World TB Day” mkoa wa Shinyanga
yamefanyika katika machimbo ya dhahabu ya Nyangarata kata ya Lunguya
halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.
Maadhimisho ya siku ya kifua
kikuu duniani yamefanyika Machi 24,2017 katika kitongoji cha
Nyangarata,kijiji cha Kalole kata ya Lunguya ambapo kuna shughuli za
uchimbaji wa madini.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na
timu ya afya mkoa wa Shinyanga na za wilaya kwa ushirikiano mkubwa wa
shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare
Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya
Ukimwi na Ukimwi katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu,Geita,Mara,Mwanza na
Tanga.
AGPAHI pia ni wadau wa muda mrefu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania.
Mgeni rasmi katika maadhimisho
hayo yenye kauli mbiu ya ‘Tuungane Kutokomeza Kifua Kikuu’ alikuwa mkuu
wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa
Shinyanga.
Awali akisoma risala katika
maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani,Meneja wa AGPAHI kanda ya
ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele alisema kutokana na ushirikiano wanaopata
kutoka serikalini wamepanua zaidi huduma za ushauri nasaha na upimaji
VVU,tiba na matunzo ya watu wanaoishi na VVU na uchunguzi wa kifua kikuu
katika maeneo ya migodi na maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo wa
madini.
Alisema hivi sasa shirika hilo
linatekeleza mradi wa kifua kikuu migodini tangu mwezi Desemba 2016
wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu kifua kikuu kwa wachimbaji pamoja
na wananchi wanaoishi maeneo hayo ili waweze kuchukua hatua za haraka
kujikinga na kupata tiba sahihi ya kifua kikuu.
“Katika kipindi cha miezi
minne ya mradi huu,jumla ya watu 2637 walifanyiwa uchunguzi wa kifua
kikuu wakiwemo wanaoendelea kuchimba na walioacha kuchimba na familia
zao,kati yao 364 walihisiwa kuwa na kifua kikuu”,alieleza Dkt. Mabelele.
Alibainisha kuwa kati ya watu
hao 364, 345 kati yao walipelekwa kwenye uchunguzi ambapo 16 wakiwemo
watoto watatu walibainika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu na hivyo
kuanzishiwa matibabu.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa
Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya alisema mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya
nne kitaifa kwa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu ambapo mikoa
inayoongoza ni Dar es salaam,Mbeya na Mwanza.
Dkt. Mpuya alizitaja sababu
zinazochangia maambukizi hayo kuwa ni wananchi kuchelewa kufika katika
vituo vya tiba,imani potofu kwa wananchi kukimbilia kwa waganga wa jadi
wakiamini kuwa wamerogwa na uhaba wa vifaa vya uchunguzi.
Aidha Dkt. Mpuya alilipongeza
shirika la AGPAHI kwa kuisaidia serikali vifaa vya kuchukulia sampuli za
makohozi,hadubini za kisasa katika vituo vya afya ikiwemo cha Lunguya
ambacho kimepewa mashine ya uchunguzi wa kifua kikuu iitwayo “Gene Xpert”.
Naye mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo ,mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliwataka
wananchi kuachana na imani potofu za kuamini waganga wa jadi na badala
yake wanapoona dalili za ugonjwa wa kifua kikuu wafike katika vituo vya
afya kupima afya zao kisha kuanza huduma ya matibabu.
Mkuu huyo wa wilaya
alitahadharisha kuwa huduma za kupima kifua kikuu na matibabu zinatolewa
bure hivyo kuwanyooshea kidole wale watakaobainika kuomba fedha kwa
ajili ya huduma hiyo ambapo alitoa agizo la maduka binafsi ya dawa za
binadamu kuacha mara moja kuuza dawa zinazotibu ugonjwa wa kifua kikuu.
Miongoni mwa shughuli
zilizofanyika wakati wa maadhimisho hayo katika machimbo ya Nyangarata
ni huduma ya kupima VVU,kufanya uchunguzi wa kifua kikuu,tohara kwa
wanaume na kuandikisha watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa ajili
ya vyeti vya kuzaliwa lakini pia shirika la AGPAHI kukabidhi baiskeli
kwa watoa huduma ngazi ya jamii wanaofanya kazi ya uchunguzi wa kifua
kikuu migodini.
Angalia
hapa matukio katika picha yaliyojiri wakati wa maadhimisho ya siku ya
kifua kikuu duniani katika mkoa wa Shinyanga kwenye machimbo ya
Nyangarata wilayani Kahama.
Katikati ni mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Msalala Simon Berege akimwongoza Mkuu wa wilaya
ya Kahama Fadhili Nkurlu aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya
siku ya Kifua kikuu duniani mkoa wa Shinyanga kwenda kukagua mabanda
yaliyokuwa yanatoa huduma za kupima VVU,uchunguzi wa kifua kikuu,tohara
na huduma zingine za afya sambamba na zoezi la kuandikisha watoto ili
wapate vyeti vya kuzaliwa
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu (mwenye suti nyeusi) na Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa Dkt.
Nkingwa Mabelele(kulia) wakisikiliza maelezo ya wataalamu wa afya katika
banda la kupimia VVU
Ndani ya banda la uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu-Wataalamu wa afya wakitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu
Zoezi la tohara kwa wanaume
linaendelea-Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akiwa
katika banda la kutolea huduma ya tohara kwa wanaume bure.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akiwa katika banda la kutolea huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma ya mama na mtoto
Kushoto ni mratibu wa huduma za maabara mkoa wa Shinyanga Muhdin Hamza akimweleza jambo mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu akizungumza na wataalamu wa afya kutoka kituo cha afya Lunguya
waliokuwa wanaendesha zoezi la kuandikisha watoto wenye umri chini ya
miaka mitano ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa
Wakazi wa Nyangarata wakiwa katika mabanda yaliyokuwa yanatoa huduma za upimaji wa VVU na uchunguzi wa kifua kikuu
Zoezi la kuandikisha watoto wenye miaka chini ya mitano ili wapate vyeti vya kuzaliwa likiendelea. Kitongoji
cha Nyangarata ambapo kuna machimbo ya madini ya dhahabu kimepewa
upendeleo wa kuwekewa kituo cha kuandikisha watoto badala ya kwenda
kwenye ofisi ya kata ya Lunguya au vituo vya afya vilivyopo katika kata
hiyo
Watoa huduma wakitoa maelezo kwa
wakazi wa Nyangarata kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu kwenye banda
lililokuwa linatoa huduma za uchunguzi wa kifua kikuu
Mchimbaji mdogo wa madini akichukuliwa damu kwa ajili ya kupima VVU
Diwani wa kata ya Lunguya
Benedict Mussa akiwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria
maadhimisho hayo ambapo alisema eneo la Machimbo ya Nyangarata ni
miongoni mwa maeneo ambayo yana watu wengi wenye ugonjwa wa kifua kikuu
ndiyo maana maadhimisho ya siku ya kifua kikuu yamefanyika hapo
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa,
Dkt. Nkingwa Mabelele akisoma risala fupi kuhusu mradi wa kifua kikuu
migodini ulioanzishwa na shirika la AGPAHI mwaka 2016 kwa lengo la
kuongeza uelewa kuhusu kifua kikuu kwa wachimbaji wa madini na wananchi
wanaoishi maeneo hayo. Mradi huo unafadhiliwa na shirika la ADPP la
Msumbiji.
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa,
Dkt. Nkingwa Mabelele alisema shirika hilo limekuwa likisaidia katika
kutoa mafunzo kuhusu huduma za kifua kikuu na UKIMWI kwa watumishi wa
afya na kutoa elimu kwa umma kwa njia ya radio na kufundisha wahudumu
katika ngazi ya jamii ili waweze kutoa huduma katika maeneo ya migodi
Wananchi wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Dkt. Mabele alieleza kuwa
shirika la AGPAHI kupitia wafadhili wake limeweza kununua na kusambaza
vitendea kazi kama vile baiskeli na vifaa vya kuchukulia sampuli za
makohozi, hadubini 8 za kisasa kwa ajili ya vituo vya afya vya
Bugarama,Lunguya,Chela,Segese,Chambo,Ushetu,Nindo na Tinde.
Dkt. Mabelele aliongeza kuwa
shirika la AGPAHI limenunua mashine moja ya uchunguzi wa kifua kikuu
‘Gene Xpert’ yenye uwezo wa kupima na kugundua uwepo wa kifua kikuu na
kutambua usugu dhidi ya dawa za kifua kikuu katika kituo cha afya
Lunguya katika halmashauri ya wilaya ya Msalala
Maafisa kutoka AGPAHI wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea eneo la tukio
Mkazi wa Nyangarata Robert
Mayinja akitoa ushuhuda baada ya kupona ugonjwa wa kifua kikuu ambapo
aliwataka wananchi kufika katika vituo vya afya kupima afya zao pale
wanapoona kuna dalili za ugonjwa wa kifua kikuu na kuhakikisha wanapata
tiba kwani ugonjwa wa kifua kikuu unatibika
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa,
Dkt. Nkingwa Mabelele akikabidhi baiskeli kwa mkuu wa wilaya ya Kahama
Fadhili Nkurlu ili awakabidhi watoa huduma ngazi ya jamii wanaofanya
kazi ya uchunguzi wa kifua kikuu katika maeneo ya migodi halmashauri ya
Msalala
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu akimkabidhi baiskeli mmoja wa watoa huduma hao.AGAPHI imetoa
baiskeli tatu ikiwa ni nyongeza ya baiskeli zingine 12 zilizokwisha
tolewa awali kupitia mradi wa kifua kikuu migodini
Mtoa huduma ngazi ya jamii anayefanya kazi ya uchunguzi wa kifua kikuu akiendesha baiskeli yake baada ya kukabidhiwa
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa
Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya akizungumza katika maadhimisho hayo ambapo
alilipongeza shirika la AGPAHI kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano
dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu
Meza kuu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Wakazi wa Nyangarata wakiwa katika mabanda ya huduma ya upimaji wa VVU na uchunguzi wa kifua kikuu
Kaimu katiba Tawala mkoa wa
Shinyanga Mohammed Nchira akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ambapo
alisema jitihada zaidi zinatakiwa ili kupambana na ugonjwa wa kifua
kikuu mkoani Shinyanga huku akiwataka wananchi kufika katika vituo vya
afya kupima afya zao na kuanza huduma za matibabu pale wanapobainika
kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani
mkoa wa Shinyanga ambapo aliwataka wananchi kuepuka kutumia muda mwingi
kwa waganga wa kienyeji kwani hawawezi kutibu ugonjwa wakifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu alisema vipimo vya kifua kikuu vinatolewa bure hivyo kuwataka
wananchi kuwafichua wanaotoza pesa kwa ajili ya huduma ya vipimo na hata
dawa za ugonjwa wa kifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu alitumia fursa hiyo pia kulipongeza shirika la AGPAHI kwa kazi
nzuri linalozifanya mkoani Shinyanga hususani katika mapambano dhidi ya
VVU na UKIMWI na ugonjwa wa kifua kikuu huku akiyaomba mashirika mengine
kujitokeza kuwasaidia wananchi wa mkoa huo
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu pia akatumia fursa hiyo kuwahamasisha wakazi wa Nyangarata
kuimarisha amani katika eneo hilo ambalo lilianza kusifika kwa matukio
ya kihalifu
Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala mheshimiwa Simon Berege akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani
Mkazi wa kitongoji cha Nyangarata akipokea zawadi ya tisheti baada kujibu maswali yanayohusu ugonjwa wa kifua kikuu
Mkazi wa kitongoji cha Nyangarata akijibu maswali kuhusu jinsi ugonjwa wa kifua kikuu unavyoambukizwa na jinsi ya kupata tiba
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
No comments :
Post a Comment