Katibu mkuu wa shirikisho la soka
barani Afrika CAF, Hicham El Amrani ametangaza kujiuzulu wadhifa wake
mwishoni mwa juma bila ya kutoa maelezo ya sababu za kufikia uamuzi
wake.
Kwa mujibu wa taarifa hii
iliyoandikwa na RFI,Amrani mwenye umri wa miaka 37 raia wa Morocco,
ametangaza uamuzi wake kupitia kwenye barua yake aliyoliandikia
shirikisho la mpira barani Afrika, CAF.
Hata hivyo wadadisi wa mambo
wanaona kuwa kujiuzulu kwake kuna uhusiano mkubwa na kuanguka kwa
aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu kwenye shirikisho hilo, Issa Hayatou,
aliyeangushwa na Ahmad Ahmad rais wa chama cha soka cha Madagascar.
Katibu mkuu huyo alikuwa
kiongozi mtiifu kwa Hayatou na mara kadhaa amekuwa akimtetea Hayatou
aliyeliongoza shirikisho hilo kwa miaka 29.
Hicham alikuwa katibu mkuu wa
muda mwaka 2010 baada ya aliyekuwa katibu mkuu Mustapha Fahmy kupelekwa
shirikisho la kabumbu la dunia Fifa.
Rais mpya wa CAF, Ahmad Ahmad
tayari amechukua rasmi ofisi kutoka kwa Issa Hayatou mwishoni mwa juma,
ambapo hii leo atakuwa na mkutano na maofisa wa shirikisho la CAF mjini
Cairo.
Rais mpya wa CAF anaonekana hata
kuwa kipenzi na rafiki wa karibu wa rais wa Fifa, Gianni Infantino
ambaye toka awali alionekana kumuunga mkono na hata kufanya ziara kadhaa
kwenye mataifa ya Afrika kujaribu kuwashawishi viongozi wamchague.
Ahmad ambaye wakati wa kampeni
zake aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwenue shirikisho
hilo, anatajwa kama mtu makini ambaye huenda akabadili sura ya
kiutendaji ya shirikisho hilo.
No comments :
Post a Comment