Saturday, February 11, 2017

WAZIRI MKUU AZITAKA TAASISI ZA UMMA KULIPA MADENI YA TTCL NDANI YA MIEZI MINNE


4G 5
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi mbalimbali za umma zinazodaiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ziwe zimelipa madeni yao ifikapo Juni 30, mwaka huu.
TTCL inazidai taasisi mbalimbali za umma jumla ya sh. bilioni 11.5 ikiwa ni gharama ya huduma walizozitoa kwa taasisi hizo, hivyo kukwamisha utendaji wa kampuni hiyo.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, 10 Februari, 2017) wakati akizindua huduma za simu ya mkononi kwa teknolojia ya 4G LTE ya TTCL mjini Dodoma.
Pia amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa akutane na wadaiwa sugu wote wathibitishe madeni husika na kisha wapange namna ya kulipa.
“Nijuavyo, kila Wizara inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za simu, sasa haya malimbikizo yanatoka wapi?. Ni lazima wadaiwa wote walipe madeni yao mara moja,” ameagiza.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “unapokuwa na deni lazima ulipe. Mheshimiwa Waziri simamia hili, na unipe taarifa ya utekelezaji  kabla ya Mkutano ujao wa Bunge la Bajeti,”.
Pia Waziri Mkuu alitoa rai kwa Menejimenti na watumishi wa TTCL kwa kuwataka watambue dhamana waliyopewa na waitendee haki  kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi.

“Fanyeni kazi kwa bidii, weledi, uzalendo, maarifa na ubunifu wa hali ya juu. Imarisheni Idara ya Masoko, hamasisheni ubunifu kwenye Kampuni na wapeni nafasi vijana wenye uwezo,”.
“Kama hiki ni kizazi cha T, wacha kizazi hicho kiongoze mapinduzi ya T, muhimu uzalendo, uwezo, dhamira na ubunifu vizingatiwe katika kutoa nafasi hizo,”. amesisitiza.
Pia amewataka viongozi wa TTCL wapitie upya muundo wake na wajiridhishe kama unaendana na ushindani wa kibiashara na dhamira ya Serikali ya kupunguza gharama zisizo za lazima.
Akizungumzia suala la idadi ya watumishi wa Kampuni, Waziri Mkuu ameshauri wajifanyie tathmini wenyewe kujua mahitaji halisi ya watumishi na kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria za nchi.
“Serikali inatarajia TTCL ijiendeshe kwa faida na sio kuja kuiomba Serikali ruzuku, hivyo hamna budi kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni kwa kadiri inavyowezekana,” amesema.
Awali, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Waziri Kindamba alisema miongoni mwa changamoto zinazokabili kampuni hiyo ni pamoja na mtaji mdogo.
Pia aliiomba Serikali iwasaidie ili waweze kulipwa madeni yao wanayozidai taasisi mbalimbali za umma kutokana na huduma walizozitoa kwa taasisi hizo.
Hata hivyo Bw. Kindamba ameahidi kwamba watafanya kazi kwa biidi ili kuhakikisha TTCL inaongoza kwa kutoa huduma bora za mawasiliano nchini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
  1. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, FEBRUARI 10, 2017

No comments :

Post a Comment