Monday, February 13, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA MAENEO YA MAGEREZA YAPIMWE


 MAJALIWA MAGEREZA CUE IN
*Ataka karakana za ujenzi, useremala zianzishwe kupunguza gharama
*Asisitiza ufyatuaji matofali kukabili upungufu wa nyumba za askari
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Malewa asimamie zoezi la upimaji wa maeneo yanayomilikiwa na Magereza kote nchini na kuhakikisha
yanawekewa mipaka.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatatu, Februari 13, 2017) katika kikao baina ya Kamishna huyo mpya na Maafisa Magereza wa Mikoa yote na maafisa wanaoshughulikia kilimo na viwanda alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma.
“Magereza yetu mengi yako kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Baadhi ya maeneo kuna migogoro kwa sababu wananchi wamejenga karibu kabisa na maeneo ya Magereza. Lazima tupime maeneo yote na kuyawekea alama mipakani ili kubainisha maeneo yetu,” amesisitiza.
Mbali ya maeneo ya Magereza, Waziri Mkuu amesema, jeshi hilo lina mashamba makubwa ambayo pia hayajapimwa hali ambayo amesema imechangia baadhi ya wananchi kulima ndani ya maeneo ya jeshi hilo.
“Natambua kuwa jeshi hili lina mashamba makubwa lakini nayo pia hayajapimwa. Kila RPO ni mjumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wake, tumieni wapima ardhi kutoka kwenye Halmashauri zenu na mhakikishe kuwa maeneo hayo yanapatiwa hati,” amesema.
Amesema umefika wakati sasa kila gereza litambue na kuainisha fursa walizonazo ili waweze kuamua ni kwa kiasi gani wanaweza kujitegemea kwa uzalishaji. “Kama ni kilimo, ufugaji, au uzalishaji wa umeme, tuangalie ni kipi kinaweza kuvutia uwekezaji, lakini cha msingi zaidi ni lazima tuwe na hati za maeneo tuliyonayo,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya magereza yalikuwa maarufu kwa kilimo lakini hivi sasa hakuna hata moja lenye trekta na kama yapo ni moja au mawili tu. “Sasa hivi teknolojia ya kilimo imebadilika, ni lazima tutumie zana za kilimo ili kwenda na kilimo cha kisasa.
Akizungumzia kuhusu ufugaji na uvuvi wa samaki, Waziri Mkuu aliagiza jeshi hilo litumie maafisa wake waliobobea kwenye sekta hizo, watumike kuendeleza na kuhamisha ujuzi wao kwa wafungwa wanaotumikia vifungo ili wanapotoka gerezani, wawe na ujuzi ambao utawasaidia kujikimu kimaisha wanaporudi kuishi vijijini.
“Nimetembelea maonesho ya Nanenane na Sabasaba huko nimekuta wamejenga banda la kuku juu ya bwawa la samaki. Hii ina maana kuku wanakula na kinyesi chao kinakuwa ni chakula kwa wale samaki walioko bwawani,” amesema.
Amemtaka Dk. Malewa aangalie uwezekano wa kuanzisha karakana na ujenzi kwenye kila gereza ili maafisa na wafungwa waliopo kule watumike kufanya kazi kwenye karakana hizo. “Nimetembelea gereza la Isanga, nikakuta kuna milango haina komeo. Kwa vile hakuna karakana, inabidi atafutwe fundi kutoka mtaani ili aje kutengeneza kitasa au komeo. Tuanzishe karakana na tuziboreshe,” amesisitiza.
Amesema uwepo wa karakana hizo ziwe ni za umeme, ujenzi au useremala, utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa jeshi la magereza kwa matengenezo madogo madogo yatafanywa na watu wa kwenye karakana badala ya kutumia watu wa nje.
Amesema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za askari, kila afisa magareza wa mkoa hana budi kuandaa matofali ya kutoka kwani timu za wafyatuaji wanazo na nguvukazi wanayo pia.
“Badala ya kutegemea wazabuni, kule kwenye udongo mzuri, tafuteni vifaa mfyatue matofali ya hydraform. Kule kwenye mchanga, fyatueni ya saruji. Kuweni na matofali ya kutosha kulingana na mahitaji yenu, mtakuwa mmepunguza gharama za ujenzi wa nyumba za askari kwa kiasi kikubwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu huyo, Dk. Malewa amesema atafuatilia suala la upimaji wa maeneo ya magereza kwa sababu wanao wapimaji na vifaa wanavyo. Amesema kuna magareza 11 yenye migogoro ya maeneo na wananchi.
“Pia tutafuatilia upimaji wa maeneo ya mashamba ya magereza. Tumeanzisha mashamba makubwa ya kilimo na tutahakikisha maeneo hayo yote yanapimwa na kuwekewa alama za mipaka,” amesema.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. William Tate Ole Nasha; Kamishna Jenerali wa Magereza, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo wanaoshughulikia Kilimo na Mifugo pamoja na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
  1. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, FEBRUARI 13, 2017.

No comments :

Post a Comment